WAZAZI WAKATAZA WALIMU WASIWAFUNDISHE WATOTO WAO JINSI YA KUTUMIA CONDOM

 
Imeelezwa kuwa Baadhi ya wazazi na walezi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamekuwa wakiwazuia walimu kutoa elimu ya njia ya kujikinga na ukimwi kwa watoto wao wa sule za msingi ikiwemo matumizi sahihi ya condom. Hayo yamebainika leo katika semina iliyoandaliwa na shirika la UNESCO iliyojumisha wakuu wa shule za msingi na sekondari pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali iliyofanyika katika ukumbi wa Golden Valley Mjini Kahama.

Akichangia hoja katika semina hiyo Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Korogwe Bi Ashura Rugakingira amesema kuwa wamekutana na tatizo hilo toka kwa baadhi wazazi hao licha ya kuwa somo hilo lipo katika mtaala wa Serikali.

Rugakingira amesema kuwa changamoto hiyo inawafanya walimu wengi kukata tamaa ya kutoa elimu hiyo ya kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa wanafunzi hao.

Awali akifungua semina hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu Bi Isabela Chilumba amewataka walimu hao kuvunja ukimya na kuwa wawazi kuzungumza na wanafunzi wao kuhusu Maambukizi ya virusi vya ukimwi na UKIMWI.

Sambamba na hayo Chilumba ametoa angalizo kwa wananchi kutodanganyika na takwimu za maandishi zinazotolewa na kwamba kila mtu awe mstari wa mbele kupima afya yake mwenyewe.

Naye Msimamizi wa mradi huo wa Elimu ya Afya ya UKIMWI, uzazi na maadili kwa vijana kutoka UNESCO Mathius Herman amesema lengo la mradi huo ni kujenga mahusiano rasmi kati ya Mashirika yasiyo ya serikali na shule.

--- Imeandikwa na William B via, KB blog
back to top