Kardinali Pengo asifia Uswisi

Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo  akisalimiana na mzee wa makamo jijini Dar es Salaam 
Pengo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, alitoa pongezi hizo jana katika misa ya maadhimisho ya miaka 50 ya kituo hicho iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, huku akiwaonya viongozi wenye nia ya kujinufaisha binafsi na kituo hicho.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameishukuru Serikali ya Uswisi kwa kulisaidia kanisa hilo, nchini kuanzisha Kituo cha Maendeleo Msimbazi ili kutoa huduma kwa maskini na jamii ya Tanzania.
Pengo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, alitoa pongezi hizo jana katika misa ya maadhimisho ya miaka 50 ya kituo hicho iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, huku akiwaonya viongozi wenye nia ya kujinufaisha binafsi na kituo hicho.
Alieleza kuwa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania Uswisi imeweza kujenga kituo hicho kilichoweza kutoa msaada ya aina mbalimbali kwa maskini na jamii bila ya kupata faida.
“Serikali ya Uswisi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania imeweza kusaidia uanzishwaji wa kituo hiki ambacho leo(jana)kimetimiza miaka 50 kwa ajili ya kutoa huduma kwa maskini na jamii kwa ujumla,”alisema.
Alisema kuwa Kituo cha Maendeleo Msimbazi hakiwezi kufananishwa na asasi za kiraia au benki za biashara kwa sababu kimejikita katika kuwasaidia wananchi wasiojiweza ili kupata msaada na kujiondoa kwenye umaskini.
Kutokana na hali hiyo, Kardinali Pengo aliwataka wananchi kutafakari mambo yaliyofanywa na kituo hicho licha ya kuwapo kwa changamoto za kibinadamu alizosema haziwezi kurudisha nyuma utendaji wa kazi zao.
Alisema kuwa kituo hicho kimeweza kutoa huduma katika kipindi chote cha misa 50 bila kuangalia masilahi binafsi, jambo lililosaidia kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii nchini.
Alibainisha, viongozi ambao walikuwa na malengo ya kujinufaisha wenyewe wameshindwa kufanya hivyo katika kituo hicho kutokana na kutofautiana malengo ya uanzishwaji wake.
Alifafanua kuwa katika ulimwengu wa sasa, shughuli za maendeleo zimeweza kuwasaidia wananchi kujiepusha na mambo mbalimbali yanayorudisha nyuma maendeleo, hivyo wanapaswa kujifunza mambo yatakayosaidia kukuza uchumi.
“Mpaka sasa tunaweza kujivunia mambo mbalimbali ya kimaendeleo yaliyofanywa na kituo hiki bila ya kupata faida, jambo ambalo linapaswa kuigwa na watu wengine,”aliongeza.
Alibainisha, kutokana na hali hiyo, wameweza kutekeleza mpango wa Yesu Kristo aliyeweza kujitoa kwa binadamu bila ya kutaka malipo au faida yoyote.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi alisema kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora
back to top