Clinton atua Dar kiaina

Rais Jakaya Kikwete akimpokea mgeni wake rais Mstaafu wa Marekani Bill Clinton anayepanda kwenye gari 
Ni kukagua miradi inayofadhiliwa na taasisi yake, wanachi wamshangilia kuingia mitaa ya watu maskini na kuzungumza nao

Dar es Salaam. Rais wa Mstaafu wa Marekani, Bill Clinton jana alifanya ziara katika makazi ya watu duni eneo la Vingunguti, wilayani Ilala Dar es Salaam, ambapo alikagua miradi midogomidogo ya wananchi inayofadhiliwa na mfuko wake (Bill Clinton Foundation).
Clinton alitembelea eneo hilo akitokea moja kwa moja Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam (JNIA), alipowasili akiwa katika ziara ya nchi mbalimbali za Afrika kukagua miradi inayoendeshwa na mfuko wake.
Katika eneo hilo rais huyo mstaafu alipokewa kwa shamrashamra mbalimbali ikiwamo ngoma za kiasili huku baadhi ya wananchi wakipigwa butwaa na kutoamini macho yao kwa kiongozi huyo kutembelea makazi yao.
Aidha, Clinton alipata wasaa wa kusalimiana na wakazi wa Vingunguti wakiwamo watoto ambao walishindwa kuzuia hisia zao wakijaribu kumsogelea, hali iliyomsukuma Clinton kuwasogelea na kuwasalimia kwa kuwashika mikono.
Maneno ya ‘Welcome Vingunguti Clinton‘ yalisisika kutoka kwa wananchi kuashiria kumkaribisha rais huyo wa 42 wa Marekani wakati alipowasalimia akitumia takriban dakika 15.
Clinton alikagua miradi ya midogomodogo ya wananchi iliyo chini ya mfuko wake ikiratibiwa na kutekelezwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Plan) pamoja na Benki ya Barclays kupitia Vikoba.
Miradi aliyokagua ni pamoja na saluni za kinamama, ushonaji na chips ambapo pia alishuhudia mmoja wa wanachama wa vikundi hivyo akikabidhiwa mkopo wa Sh100,000 ambaye alieleza mbele ya Clinton kuwa atazitumia kwa mradi wa maandazi, hali iliyomfanya rais huyo na umati wa watu uliohudhuria kucheka.
Akizungumza katika ziara hiyo Clinton alizishauri benki nchini, kuwekeza kwenye vikundi vya kuweka na kukopa (Vikoba) akieleza kuwa ndiyo mkombozi kwa wananchi hasa wanawake.
“Nimekuwa kwenye miradi hii kwa miaka 30 kabla sijawa rais, hivyo basi najua umuhimu wake. Benki zinatakiwa zisaidie Vikoba kwani vikundi hivyo huwafikia wananchi kwa haraka na wepesi hivyo basi kunahitajika njia mbadala za kuhakikisha vinakuwa imara,” alisema Clinton na kuongeza;
“ Raha ya maendeleo ni kuona watu wanajitegemea wenyewe katika shughuli za kujiingizia kipato.”
Mmoja wa wananchi walionufaika, Zainab Paul ambaye ni mwanachama wa Kikundi cha Amani Hisa alisema kuwa kupitia Mfuko wa Bill Clinton na Vikoba ameweza kujikwamua kimaisha ikiwamo kumlipa mtoto wake karo ya shule.
“Kikundi chetu kina wanachama 30 na huwa tunanunua hisa kwa Sh2000 na kila mwanachama anaruhusiwa kukopa zaidi ya mara tatu,” alisema Paul.
back to top