Wanafunzi 5,000 washindwa kuingia vyuo vikuu

Wanafunzi wa shule ya sekondari nchini wakiwa kwenye mahafali ya kuhitimu kidato cha sita.
Pazia la udahili huo kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu, lilifungwa rasmi Julai 5, mwaka huu. Hadi wakati unafika tarehe hiyo, wanafunzi waliokuwa wameomba nafasi hiyo ni 39,140.
Dar es Salaam. Siku chache baada ya kufungwa kwa pazia la udahili kwa wanafunzi wa kidato cha sita walioomba kujiunga na vyuo vikuu nchini, imebainika kuwa zaidi ya wanafunzi 5,000 wameshindwa kujiunga na vyuo hivyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo matumizi ya mtandao wa kuomba udahili.
Pazia la udahili huo kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu, lilifungwa rasmi Julai 5, mwaka huu. Hadi wakati unafika tarehe hiyo, wanafunzi waliokuwa wameomba nafasi hiyo ni 39,140.
Matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, yanaonyesha kuwa watahiniwa 50,611 walifanya mtihani huo na kati yao 44,366 sawa na watahiniwa wa shule waliofaulu ni 40,242 sawa na asilimia 93.92 ya waliofanya mtihani huo.
Watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani huo walikuwa ni 7,659 na waliofaulu ni 4,124 sawa na asilimia 53.87. Kutokana na matokeo hayo, watahiniwa wote waliofaulu ni 44,366, hivyo kufanya wanafunzi walioshindwa kujiunga na vyuo vikuu kuwa 5,226.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi, Mkurugenzi wa Ithibati na Ubora wa Elimu ya Juu wa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), Dk Savinus Maronga alisema, wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kuomba kujiunga na vyuo vikuu ni 39,140 na kwamba vyuo vikuu nchini vina uwezo kwa kuchukua wanafunzi 60,000.
Dk Maronga alisema hali hiyo inatokana na baadhi yao kutokuwa na sifa zinazotakiwa kuweza kuomba udahili wa kumwezesha kusoma elimu ya juu.
“Kuna baadhi hawana sifa ‘Eligibility’ za kuweza kuchaguliwa kuingia Chuo Kikuu. Hivyo ili uweze kudahiliwa kuendelea na elimu ya juu ni lazima uwe na vigezo. Kuhusu mfumo sidhani kama ulikuwa na matatizo yeyote,” alisema Dk Maronga
Kauli za Wanafunzi
Wanafunzi waliozungumza na gazeti hili kuhusu mfumo huo wa udahili wa mtandao, walisema una usumbufu kutokana na wengi kutokujua kuutumia.
Frank Mabagala aliyehitimu Shule ya Sekondari Pugu Jijini Dar es Salaam, alisema wanafunzi walio wengi wameshindwa kuutumia mfumo huo kwani una mambo mengi ya kufanya.
“Nilijaza fomu vizuri tu, lakini sikuwa najua kama kuna wakati nilitakiwa kwenda kuangalia ‘Eligibility’ hadi nilipoambiwa na rafiki yangu kwenda kuangalia ‘Eligibility’ na kukuta kuna nafasi imeandikwa ‘NO’ hapana vyuo vyote nilivyochagua,” alisema Mabagala.
Alisema hata upatikanaji wa vocha za TCU bado zilikuwa tatizo, kutokana na kupatikana sehemu moja tu ya Benki ya NBC. Hivyo kwa watu wanaoishi pembezoni mwa benki hiyo kuwawia vigumu kupata huduma hiyo kwa haraka.
back to top