Tanzania kupigiwa kura maajabu ya asili Afrika

Mt Kilimanjaro


Tanzania imechaguliwa kuwa kati ya nchi zilizoshinda na vivutio vyake zaidi ya kimoja ambavyo vitakuwa miongoni mwa maajabu saba ya asili barani Afrika baada ya kukamilika kwa upigaji kura katika shindano la kutafuta maajabu saba ya asili barani Afrika lilomalizika Desemba 31, mwaka jana.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB)  Dk. Aloyce Nzuki, inasema kuwa kuwa Taasisi ya Seven Natural Wonders ambayo ilikuwa ikiendesha shindano hilo imewasilisha ripoti kwa Mkurugenzi wa TTB na kusema kuwa  Tanzania itakuwa ni miongoni wa nchi ambazo angalau moja ya vivutio vyake kitaingia katika orodha ya maajabu saba ya asili barani Afrika.
Taasisi hiyo  ilisema kuwa Tanzania  itakuwa mwenyeji wa sherehe za tukio la utangazaji wa vivutio vilivyoshinda katika shindano hilo na itakuwa fursa kwa Watanzania na Afrika kwa ujumla kufurahia tukio hilo.
“Bodi ya Utalii inapenda  kuwashukuru watu wote wa ndani na nje ya  Tanzania walioshiriki katika kupigia kura vivutio vya Tanzania  ambapo  Bonde la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mlima Kilimanjaro vilikuwa katika shindano hili,” alisema.
Sherehe za utangazaji wa washindi zitafanyika jijini Arusha Februari 11, mwaka huu na watu mashuhuri  kutoka nchi mbalimbali Afrika, waandishi  kutoka vyombo vya habari vya kimataifa na ndani ya nchi wataalikwa kushiriki na kushuhudia utangazaji wa vivutio vya Kitanzania na vingine vya Afrika kuwa  maajabu saba ya asili barani Afrika.
back to top