Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis ametimiza mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo.
Katika miezi yake 12 ya uongozi, Papa Francis amefanya mambo kadhaa
muhimu ambayo watangulizi wake walishindwa kuyafanya, huku akitoa
kipaumbele katika ujenzi wa kanisa hilo katika maeneo yenye ongezeko
kubwa la watu na kuwajali masikini.
Papa Francis aliingia madarakani Machi 13, 2013 na kupewa nafasi ya
kuliongoza kanisa hilo lenye zaidi ya waumini bilioni 1.2 duniani.
Miongoni mwa mambo yasiyo ya kawaida aliyofanya baada ya kuchaguliwa, ni pamoja na kukataa kutumia gari maalumu kwa ajili yake.
Gari hilo lilikuwa limefunikwa kwa kioo, hivyo kukiuka utaratibu wa
awali uliowekwa na Kanisa wa kuwalinda viongozi wao wakuu baada ya Papa
John Paul II kupigwa risasi.
Pia Papa Francis aliwahi kusafiri katika basi moja na makadinali. Kama
haitoshi, pia alikataa kutumia gari aina ya Mercedes, badala yake
alitumia gari aina ya Renault iliyokuwa na miaka 20, huku ikiwa
imetembea zaidi ya kilomita laki mbili.
Akielezea aina ya uongozi wake, mwandishi Chris Boeskool anasema uamuzi
huo siyo tu ni wa hatari kwa usalama, bali unaonyesha ni namna gani
asivyojali kuhusu kifo.
Pia, Papa Francis anaamini kuwa kufanya jambo zuri ni bora kuliko kuamini jambo hilo na kuishia kulisema tu.
“Bwana ametukomboa sisi sote, siyo Wakatoliki peke yao wanaoamini kuwapo kwa Mungu na wasioamini,” aliwahi kusema.
Pamoja na umri wake mkubwa, Papa Francis amekuwa mtumiaji mzuri wa
mitandao ya kijamii. Kwa mfano, akaunti yake ya mtandao wa Twitter ina
watu zaidi ya milioni tatu wanaomfuatilia duniani kote.