Bagamoyo. Mbwembwe
na tambo za kisiasa pamoja na shamrashamra mbalimbali zimetokea jana
katika Ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Chalinze baada ya
wagombea ubunge jimbo hilo kurejesha fomu zao za uteuzi wa ubunge.
Mgombea wa kwanza kurejesha fomu ni mteule wa Chama cha Wananchi CUF,
Fabian Skauki ambaye alifika saa 5.37 asubuhi na Msimamizi wa Uchaguzi
wa jimbo hilo, Samwel Sarianga alizithibitisha kuwa hazina dosari
yoyote.
Saa 7.46 mgombea wa CCM, Ridhiwan Kikwete naye aliwasili kwenye ofisi
hiyo kurejesha fomu zake, huku akisindikizwa na umati mkubwa wa
wanachama akiwamo hasimu wake wa kura za maoni, Iman Madega.
Wagombea wengine waliorudisha fomu zao ni pamoja na Chadema waliowasili
ofisini hapo huku mgombea wao Mathayo Torongey akisindikizwa kwa nyimbo
na ngoma za asili na makada wa chama hicho. Wengine ni wa Chama cha AFP,
Ramadhan Mgaya aliyerudisha saa 9:45, huku mgombea wa NRA, Muniru
Hussein akirudisha saa 9:55.