THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi)
Office of the Secretary General
Party Headquarters,
P.O. Box 3637, Zanzibar, Tanzania
E - mail: cufhabari.co.uk
Homepage: www.cuftz.org
Our Ref:
CU/HQ/KR/HUM/181
Date: 11/03/2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ukweli utaendelea kubaki ulimwenguni kwamba Zanzibar ni Nchi iliyokuwa
huru tangu asili na zama, ambayo ikitegemea raslimali zake za ndani kwa
kujiendesha katika nyanja zote za kimaisha.
Ukweli huu katu hauwezi kuondoshwa na uoni au uelewa finyu wa watu,
ambao baadhi yao wanajiita wasomi, kwa sababu ya kuchunga utashi
binafsi, maslahi, itikadi, ubabaishaji, upotoshaji wa makusudi na
matakwa ya taasisi wanazozitumikia.
Si sahihi hata kidogo na pia ni upotofu uliodhahiri kudai ati Uchumi wa Zanzibar unategemea Bara na kwamba mchango wake katika Muungano ni sawa na hakuna au pia uwezo wake wa kulipa madeni ya mikopo ni shaka tupu.
Huo ni upotofu na upotoshaji wa makusudi unaolenga kuwababaisha
wananchi, hasa wa Visiwa vya Unguja na Pemba, ambao sasa wanaelewa nini
wanachokihitaji; ni azma pia ya kuwazuga Wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba, hasa wale waliodhamiria kupigania Muungano wenye maslahi kwa
pande zote za Jamhuri za Tanzania.
La msingi ni kwamba wasiibuke watu wakajaribu kuwalisha maneno au
kuwapumbaza Wazanzibari waliokwishajifunza vyema na kuikubali Historia
kubwa ya Dola yao Huru yenye utajiri na iliyoheshimika Duniani, ambayo
hatimaye imefikia pabaya kwa kile ambacho hadi sasa wanahoji iwapo huo
unaoitwa Muungano wa Mwaka 1964 ulikuja kwa azma ya kuinufaisha au
kuidhoofisha Zanzibar.
Lazima ieleweke kwamba kinachojadiliwa hapa siyo haja ya kuwa au
kutokuwa na Muungano, bali la msingi ni kuwepo fungamano lenye kuheshimu
na kuthamini nafasi za kila muhusika, iwe Jamhuri Huru ya Tanganyika na
pia Jamhuri Huru ya Zanzibar, zilizodhihiri pasi na ghilba wala
jinamizi au azma mbaya zilizofichikana; na hapo ndipo waliposimama
Wazanzibari waliowengi katika kuelekea Mabadiliko ya Katiba, na siyo
ubabaishaji wa watu wanaojiita wasomi wa kuwaziba macho watu wa Nchi
hii.
Hapa hoja ni jee Zanzibar ilimtegemea nani kabla ya kuungana na
Tanganyika; au ilishindwa kwa kiasi gani kulipia Uwanachama wake wa
Jumuiya mbali mbali za Kimataifa, mathalan Kiti Chake cha Umoja wa
Mataifa na Jumuiya ya Madola; au ilidaiwa na nani deni lisilolipika?
Katika kuepusha uzandiki na pia kujaribu kurejesha heshima ya Nchi hii,
ambayo kwa kiasi kikubwa ilipotelea ndani ya kile kinachopewa kila aina
ya majina, mara kero za Muungano mara jinamizi mara kiini macho au
vyenginevyo, Serikali za Awamu zote zilizopita za Uongozi wa Zanzibar
ziliwahi kuwasilisha Waraka zilizojaa mapendekezo ya kujivua kutokana na
pingu hizo za kudhoofisha.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuyaondoa Mambo yote yaliyowekwa
kinyemela baadhi yao, katika hiyo inayodaiwa kuwa Orodha ya Mambo ya
Muungano, ambayo ni pamoja na Mafuta na Gesi Asilia, Elimu ya Juu,
Posta, Mawasiliano ya Simu, Kodi ya Mapato, Biashara ya Nje, Ushuru wa
Bidhaa (Excise Duty), Usafiri wa Anga, Takwimu, Tafiti, Ushirikiano wa
Kimataifa, Mambo ya Nje, Leseni za Viwanda, Polisi na Usalama.
Tena kwa azma njema, Waraka hizo zote kutoka Serikali ya Zanzibar ya
Awamu tofauti, zilisisitiza mambo muhimu ya kuulinda Muungano, yakiwemo
Masuala ya Muungano kulindwa kwa Misingi ya Katiba na Sheria badala ya
'sumu' ya siasa na maelewano (good will); Muungano kuwa na maeneo
machache yanayoweza kusimamiwa na kutekelezwa kwa urahisi kisheria;
Muungano kuainisha wazi wazi washirika wake wakuu, mipaka na haki zao;
Muungano kutoa fursa sawa za kiuchumi kwa pande zote mbili (Tanganyika
na Zanzibar); na pia ulazima wa kuwa na Muungano unaoweza kuhimili
mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.
Suala hapa ni jee ugumu ulikuwepo wapi wa kutekeleza mapendekezo hayo
yaliyokuwa na azma njema ya kujenga Muungano wa dhati wenye heshima; au
kilichosubiriwa ni hiki kisingizio cha sasa cha watu wanaojiita wasomi
na ambao wangeliweza kuwa tegemeo la Taifa, wakidai ati Zanzibar haina
uwezo wa kujitegemea au kulipa madeni; ni nini hicho kama si kupotoka au
kupotosha kwa makusudi?
Kinachohitajika hapa siyo kuwasilisha tena data za namna ambavyo
Zanzibar imekuwa ikidhoofika siku hadi siku kutokana na mfumo usiofaa au
azma iliyofichikana ndani ya Muungano; Waswahili wanasema "mwenye macho
haambiwi tazama", na kwa msomi mwenye uoni hasa, ataamini namna
Wazanzibari walivyodhoofika kwa kubebeshwa mazigo ya madeni na mikopo
isiyokuwana tija, tena ambayo sehemu kubwa inaangukia mikononi mwa
mafisadi.
Chama cha Wananchi, CUF, na kama ilivyo kwa Wazanzibari wengi, au hata
Watanzania waungwana kwa ujumla, hakiamini na katu hakitoamini kwamba
ati "Serikali Mbili haziepukiki".
Chama cha Wananchi, CUF, kinatoa wito kwa waungwana nawapenda haki,
sambamba na Wajumbe wote wa Bunge la Katiba, kusimama juu ya hoja ya
kudai Katiba yenye maslahi na Muungano wenye heshima, inayozingatia
maoni, mapendekezo na mahitaji ya umma wote, pasi na kukubali
kubabaishwa au kupotoshwa kwamba ati Zanzibar haina uwezo wa
kujitegemea.
HAKI SAWA KWA WOTE
...................................................
Salim Bimani,
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar
Headquarters:
P.O. Box 3637, Zanzibar, Tanzania
Tel: 024 22 37446
Fax: 024 22 37445
Main Office:
P.O. Box 10979, Dar-es-Salaam, Tanzania.
Tel. 022 861009
Fax: 022 861010
Directorate of Information and Policy Dissemination
The Civic United Front (CUF)
Party Headquarters
P.O. Box 3637
Zanzibar
Tanzania
Tel. (+)255 (0)747 414100 / (+)255 (0)741 257 665
E-mail: cufhabari@yahoo.com
Website: www.cuftz.org
