SERIKALI MAMBO HADHARANI

 
Rais Jakaya Kikwete.
MABADILIKO yanatarajiwa kufanyika nchini kuhusu suala zima la uwazi katika uendeshaji wa Serikali huku ikitarajiwa mambo mbalimbali ikiwemo mishahara kutokuwa siri. Rais Jakaya Kikwete alisema juzi mjini hapa, kwamba mabadiliko hayo si kwa sekta ya umma pekee, bali pia binafsi ambako kila anayejihusisha na umma hususani mashirika yasiyo ya serikali (NGO), anapaswa kuweka wazi vyanzo vya mapato, kiasi cha fedha alichopewa na matumizi yake.

Katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari wa vyombo vya Tanzania, Rais alisema ingawa ipo changamoto ya kubadili mazoea yaliyopo ya kila kitu serikalini kuendesha kwa usiri, anaamini mabadiliko yatakuwapo ndani ya miaka miwili ijayo na hadi anatoka madarakani 2015, kila kitu katika uendeshaji Serikali kitakuwa wazi.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa Mpango wa Pamoja wa Uendeshaji Serikali kwa Uwazi (OGP) ulioanzishwa na Rais wa Marekani, Barack Obama na Tanzania kujiunga nao mwaka 2011. Rais Kikwete na ujumbe wake, alikuwa hapa kuhudhuria mkutano wa mwaka wa OGP ulioanza Oktoba 31 na kumalizika jana.
Mkutano huo ulihudhuriwa na washiriki 1,000 kutoka nchi 60 wanachama na Rais Kikwete alipata nafasi ya kuueleza mkutano huo, namna Tanzania ilivyoanza utekelezaji wa masharti ya mpango huo.
“Mshahara hauwezi kuwa siri. Si ipo kwenye bajeti za Serikali?” Alijibu Rais Kikwete alipoulizwa kama suala la mishahara litaendelea kuwa siri katika utekelezaji wa mpango huo. Kikwete alisema:
“Changamoto iliyopo ni kwamba mpango huu unabadili mazoea yetu ya kufanya kazi. Sisi katika kila serikali kila kitu ni siri. Sasa OGP inataka mambo haya yawe wazi; ifike hatua mtu aone kutoa habari ni wajibu.” Alisema alifurahi Rais Obama alipomwambia Tanzania ina sifa ya kujiunga na umoja huo.
Alisema aliona ni jambo jema serikali iliyo chini ya wananchi kujiendesha kwa uwazi tofauti na mfumo uliotawala ambao ni wa usiri. Kibano halmashauri Miongoni mwa hatua za utekelezaji wa mpango alizotaja Rais Kikwete, ni pamoja na uwazi kwenye bajeti ya serikali.
Pia halmashauri zote za wilaya, miji na manispaa zinapopokea fedha kutoka serikalini, zinapaswa kubandika ukutani wananchi wasome wafahamu kiasi kilichopokewa. Vivyo hivyo kwa upande wa shule, fedha zinazotolewa zinapaswa ziwekwe wazi kwa wananchi.
Kwa upande wa vituo vya afya na zahanati, Rais Kikwete alisisitiza ni lazima dawa na vifaa tiba vinavyopelekwa, taarifa ziwekwe wazi kwa kubandikwa ukutani ili kuwezesha wananchi kufahamu aina na kiwango kilichofikishwa.
Udhibiti rushwa Uwekezaji katika Mkongo wa Taifa, ni hatua nyingine ambayo Rais alisema utasaidia kuendesha Serikali kwa uwazi.
Alisema lengo ni mkongo huo ufike kila ofisi ya wilaya jambo ambalo litarahisisha mawasiliano.
“Mkongo ukishafika, hakuna haja ya mtu kusafiri. Hata aliye Ngara (Kagera) hatakuja Dar es Salaam, tutafika mahali tutapunguza ulazima wa kwenda kwenye ofisi na hii itapunguza virushwa rushwa hivi,” alisema. Aliendelea:
“Tunafikiri kwa upana tutafika mahali, unakwenda tu kwenye mtandao unapata maelekezo au unajaza fomu badala ya kusafiri.” Usalama wa nchi Akizungumzia sheria inayotarajiwa kutungwa ya uhuru wa kupata habari, Rais alisema kuwapo kwake hakumaanishi kuruhusu pia taarifa za usalama wa nchi kuanikwa.
“Hata nchi zilizoendelea kidemokrasia…nenda uulizie kituo cha nyuklia kiko wapi, watakufunga tu…umepata taarifa kwamba leo kutakuwa na shambulio la kigaidi, halafu unatangaza kwamba leo kutakuwa na shambulio, Serikali haziendeshwi hivyo,” alisisitiza.
Wakati huo huo, Rais Kikwete alisema asasi zisizo za Serikali (AZISE) pia zinawajibika kujiendesha kwa uwazi; yasidhani kwamba uwazi ni kwa Serikali pekee.
Alisema wanaoshughulika na umma lazima wawe wawazi kwa maana kama ni fedha, wanapaswa kuweka wazi zimepatikanaje na zinatumikaje.
“Wasidhani kwamba uwazi ni upande mmoja. Masharti haya (ya OPG) ni kwa pande zote...lazima useme fulani kanipa kiasi hiki, nimetumia hivi. Kila mmoja awajibike wasidhani ni serikali tu.”
Akisisitiza nafasi ya Serikali katika kutambua na kuthamini kazi ya AZISE, Rais Kikwete alisema hivi sasa zipo takribani 18,000 na serikali haina tatizo nazo. Pamoja na kutaja kuwa kuna kazi ya kuondoa mazoea yaliyojengeka miongoni mwa watumishi wa serikali, ya kila kitu kufanywa siri, Rais alisema changamoto nyingine ni ufuatiliaji wa wananchi kusoma taarifa zinazotolewa.
Alitoa mfano wa hatua ya sasa ya Hazina kuweka hadharani fedha inazopeleka kwenye halmashauri, kwamba kuna watu hawafuatilii hata kuzisoma kwenye vyombo vya habari.
"Akishika gazeti, anasoma vichwa vya habari tu au anageuza upande wa nyuma wa gazeti," alisema na kuhimiza umma kujenga utamaduni wa kusoma na kufuatilia taarifa za fedha zinazotolewa.
 
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, ifikapo mwaka 2015 atakapoondoka madarakani, mambo mengi ya Serikali yatakuwa hadharani. Matarajio yake ni kwamba Serikali itakuwa na uwazi kuliko ilivyo sasa. Shughuli za Serikali zitaendeshwa kwa uwazi na wananchi watajua kila kitu wanachopaswa kufahamu. “Tunaanza, tutafanikiwa tu,” alisisitiza Rais Kikwete.
CHANZO NI HABARI LEO
back to top