Kiongozi wa kundi la wapiganaji la Taliban nchini Pakistan, Hakimullah Mehsud, ameuawa kwa kutumia ndege zisizokuwa na rubani, hii ni kwa mujibu wa afisaa mmoja mkuu wa kundi hilo.Shambulizi hilo lililenga gari alimokuwa anasafiria Mehsud, Kaskazini Magharibi mwa Waziristan.Watu wanne waliokuwa wanasafiri na Mehsoud wakiwemo walinzi wake wawili waliuawa katika shambulizi hilo.
Marekani pamoja na Pakistan zimewahi kudai siku za nyuma kumuua Mehsoud ingawa madai yao hayakuwa na ukweli.
Serikali ya Pakistan imetoa taarifa kulaani vikali mashambulizi ambayo Marekani inafanya kwa kutumia ndege zisizo na rubani, ikisema kuwa mashambulizi kama hayo yanakiuka uhuru wa taifa hilo.Shambulizi hilo lililofanywa siku ya Ijumaa, lililenga gari la Mehsud.
Afisaa mmoja mkuu wa ujasusi nchini Marekani, aliambia shirika la habari la Associated Press kuwa Marekani ilipokea taarifa muhimu kuthibitisha kifo cha Mehsoud.
Hata hivyo msemaji wa baraza la usalama wa kitaifa la Marekani, alisema kuwa hawawezi kuthibitisha taarifa hizo lakini ikiwa ni kweli basi ni pigo kubwa sana kwa Taliban.
Hakimullah Mehsud alijulikana sana mwaka 2007 kama kamanda wa mwasisi wa kundi hilo Baitullah Mehsud, alipowakamata wanajeshi 300 wa Pakistani .
CHANZO NI BBC SWAHILI