WANAOFANYA BIASHARA YA NGONO KAHAMA WAOKOLEWA KWA UJIO WA HUHESCO.
Zaidi ya wanawake tisini wanaofanya biashara ya ngono wilayani Kahama
mkoani Shinyanga wanatarajia kunufaika na mradi mpya wa kuwakomboa
kutoka kwenye biashara hiyo, unaoratibiwa na HUHESO Foundation kwa
ufadhili wa Rapid Funding Envelop (RFE).Hayo yameelezwa leo na
Mkurugenzi wa shirika hilo Juma Mwesigwa wakati wa utambulisho wa mradi
huo kwa wadau na waandishi wa habari katika kikao kilichofanyika katika
ukumbi wa Kaltas mjini Kahama.
Mwesigwa amesema lengo la mradi
huo ni kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI na kuwaondoa wanawake
wanaofanya biashara ya Ngono wilayani humo. Mwesigwa amesema kuwa
wanawake arobaini watapatiwa mafunzo ya cherehani na baada ya mafunzo
kila mmoja atapatiwa cherehani yake mpya huku wengine hamsini wakipatiwa
mafunzo ya ujasiriamali.
Awali akizinduwa rasmi mradi huo, Kaimu
mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Kahama Lucas Makurumo aliwata
wananchi kuupokea na wakina dada wajiunge pasipo woga kwa faida zao na
Taifa kwa ujumla.
Mradi wa kuwakomboa wanawake wanaofanya
biashara ya ngono wilayani Kahama utakaotekelezwa ndani ya mwaka mmoja
unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi milioni 146. Mradi huo
utatekelezwa katika kata Malunga, Mohongolo, Kahama Mjini, Nyihogo,
Nyasubi, Nyahanga, Majengo, Mwendakulima, Kagongwa na Mungula.