UCHAGUZI ZIMBABWE ULIKUWA HURU - OBASANJO

 
Kura za uchaguzi zikihesabiwa mjini Harare nchini Zimbabwe.
Mkuu wa ujumbe wa uangalizi kutoka Muungano wa Afrika nchini Zimbabwe, Olusegun Obasanjo amesema uchaguzi mkuu wa Jumatano ulikuwa huru na haki. Matokeo ya awali yanaonyesha Rais Robert Mugabe na chama tawala cha Zanu PF wanaongoza kwa kura nyingi

Zanu PF tayari kimedai ushindi na kupitia kwa msemaji wake, Rugare Gumbo ni kwamba kinatarajia ushindi wa asilimia 70 ya kura zote.
Lakini mpinzani wa Mugabe, Morgan Tsvangirai, amesema uchaguzi huo ni wa uongo na kusema udanganyifu uliofanyika una maana uchaguzi huo haukubaliki.
Waangalizi kutoka Umoja wa Afrika na jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika wanatarajia kutoa tamko rasmi hii leo kuhusu uchaguzi huo.
Bw. Obasanjo amesema kulikuwa na visa kadhaa wakati wa shughuli ya kupiga kura. Hata hivyo amesema visa hivyo haviwezi kutajwa kuwa na uzito wa kubatilisha au kufuta matokeo ya kura.
Msimamo wa Muungano wa Afrika unatofautiana na ule wa kundi la uangalizi la Zimbabwe Election Support Network.
Kundi hilo ambalo ndilo kubwa zaidi linalochunguza kura ya Zimbabwe limekashifu uchaguzi mkuu na kusema ulikuwa na dosari nyingi. Hii ni kwa sababu watu milioni moja walizuiwa kupiga kura.
Huku upande wa Rais Mugabe akiitangaza kushinda uchaguzi na Morgan Tsvangirai akipinga ni dhahiri kwamba Zimbabwe ingali na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa.

CHANZO: BBCSWAHILI
back to top