"Mimi nikiwa kama mtaalam wa kutatua migogoro suala la mazungumzo ni njia moja ambayo huwa inatumika mara kwa mara na inasaidia kuleta amani," alisema na kuongeza;
"Kutumia mtutu wa bunduki haileti tija kwa mataifa yote mawawili, hivyo ni busara itumike njia ya mazungumzo."
Alitoa mwito kwa nchi jirani kushirikiana kutatua mgogoro uliopo kwa njia ya mazungumzo baina ya Rwanda na DRC.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitivo cha Elimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Kitila Mkumbo, alisema anakubaliana na kauli ya Rais Kikwete na anashangazwa na Rais Kagame ni kwa nini anachukizwa kuambiwa azungumze na waasi.
"Maana yake inaonekana hataki kushauriwa...ushauri huo ni kitu kizuri kinaweza kuleta maelewano," alisema Dkt. Mkumbo. Alisema Rais Kagame, anaonekana kama dikteta kutokana na kukataa kuambiwa ukweli na viongozi wenzake.
Alisema kauli ya Rais Kikwete, aliyoitoa kwenye hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa saba hakugusia masuala ya vita na anaamini kwamba kwa karne hii sio mwafaka nchi kuingia kwenye vita kwani nchi zina matatizo mengi ambayo yanahitajika kupatiwa ufumbuzi.
"Alichoongea Rais Kikwete, ni msimamo unaotakiwa kuungwa mkono na Watanzania kwani yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu na hiyo ndiyo kauli ya nchi...hivyo alichosema ni sawa," alisema Dkt. Mkumbo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, alisema ameridhishwa na kauli ya Rais Kikwete, kwani ametumia lugha sahihi katika kueleza hali halisi, hivyo Watanzania wote wanatakiwa kumuunga mkono.
Alisema kwa hali ilivyo ni lazima Watanzania waungane katika masuala kama hayo ili kuleta mshikamano wa nchi.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Augustino Mrema, alisema anamuunga mkono Rais Kikwete, kwa kauli yake hiyo.
Alisema Rais Kagame ameanza chokochoko dhidi ya Tanzania na kwamba hivyo, ndivyo alivyoanza hata Idd Amin. "Siungi mkono vita vitokee, lakini kama atatuchokoza basi tuwe wa mwisho kujibu mapigo," alisema Mrema.
Aliyekuwa Mhadhiri UDSM, Dkt. Azaveri Lweitama, amezitaka nchi za Afrika Mashariki kukaa chini ili kuangalia jinsi ya kutatua mgogoro huo.
Alisema kuipiga Rwanda ni kazi ndogo sana, lakini hauwezi kumaliza tatizo kwa kutumia bunduki na badala yake ni vyema nchi hizo zikaangalia namna ya kumaliza mgogoro.
"Unajua mnaweza kuingia katika vita mkamuondoa Rias wa Rwanda, lakini bado mkatengeneza matatizo mengine kwa rais ajaye," alisema.
Alisema Kongo kuna waasi wa Rwanda na hata Rwanda pia kuna waasi wa kutoka Kongo, hivyo ni lazima kutafuta njia nzuri ya kutatua tatizo hilo.
Kwa upande mwingine, Dkt. Lweitama, alivitaka vyombo vya habari kutopotosha taarifa zinazozungumzia vita vikitokea hakuna mtu atakayebaki salama.
"Vyombo vya habari vijitahidi kuandika habari zisizo za uchochoezi, kwani hata ninyi pia ni Watanzania, naamini vita ikitokea hakuna mhariri wala mwandishi atakayebaki salama," alisema.
Alisema vyombo vya habari pia vina nafasi ya kukaa chini na kutafakari namna ya kumaliza mgogoro kwa kuwa vina nafasi kubwa kwa mustakabali wa taifa.
Uhusiano wa Tanzania na Rwanda unaelekea kupata mtikisiko baada ya Rais Kikwete kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa nia njema kwa kuwa bado anaamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike.
Ushauri ule aliutoa pia kwa Serikali ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda. ambapo katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli hiyo.
Tangu atoe ushauri huo viongozi wa Rwanga wamekuwa wakitoa kauli za kejeli dhidi ya Tanzania na Rais Jakaya Kikwete. Katika hotuba yake Rais Kikwete, alisema uhusiano wa Tanzania na Rwanda unapitia katika kipindi kigumu
-MAJIRA.