MABINTI WA KIZARAMO NA MAFIGA MATATU-DHANA ILIYOPOTOSHWA NA WAHUNI....

Inaamini kwa watu wengi kwamba, wasichana wa Kizaramo wanapowekwa ndani, hufundishwa kwamba, wakiingia kwenye ndoa ni lazima wawe na mafiga matatu. wanaoamini hivyo wanabainisha kuwa mafiga hayo matatu ni ishara ya wanaume watatu, yaani MUME, HAWARA MPYA na BWANA WA ZAMANI. lakini pia wapo wanaodai kwamba mafiga hayo matatu ina maana ya kuolewa mara tatu katika maisha yake. Hii ikiwa na maana kwamba, mwanamke wa kizaramo ni lazima aolewe na kuachwa mara tatu maishani mwake.

Tafsiri hiyo ni uhuni tu wa watu wachache wanaotaka kupotosha watu, lakini hakuna ukweli wowote kuhusiana na madai hayo. Ni kweli kwamba wasichana wanawali wa Kizaramo hufundishwa kuhusu mafiga matatu pale wanapokuwa wamewekwa ndani kwa ajili ya kufundwa kwa mujibu wa mila na desturi za kizaramo. Lakini mafiga hayo matatu huwakilisha watu tofauti na sio mume, hawara mpya wala bwana wa zamani, ni uzushi tu na uhuni wa watu wachache wanaopenda kudhalilisha mila za wenzao.

Mafiga matatu yanaozungumziwa, huwakilisha, watu muhimu kwenye maisha ya ndoa ya mwanamke yeyote. Figa la kwanza ni MUME, figa la pili ni NDUGU WA MUME, yaani mawifi na mashemeji zake, figa la tatu ni WAZAZI WA MUME, yaani wakwe.

Msichana wa kizaramo anapokuwa katika kufundwa, huelekezwa namna anavyotakiwa kuishi na watu hao, yaani mafiga hayo matatu. Anafundishwa namna ya kumtendea mume wake katika mazingira tofauti, hufundishwa namna ya kuishi vizuri na wakwe zake, na namna anavyoweza kuwakabili mawifi na mashemeji zake kwenye mazingira yote.

Ni kawaida ya Wazaramo kuwafundisha watoto wao wa kike namna ya kuweza kuishi na ndugu za watakaokuwa waume zao. Msichana wa Kizaramo anatakiwa kufahamu namna ya kutumia mafiga hayo bila figa lolote kuondoka, kwa sababu kama litaondoka figa moja, hataweza kubandika chungu katika mafiga yaliyobaki. Hii ina maana kwamba, bila kuwa na uelewano na na wote hao watatu, ndoa yake inaweza kuwa katika matatizo.

Ukweli ni kwamba, wasichana wa Kizaramo ambao wamezingatia kweli kile walichofundishwa, wakati wanafundwa, hutokea kuwa wanawake waadilifu sana, kuliko inavyodhaniwa. kuna ushahidi wa kutosha kwa wanawake wengi wa kizaramo ambao wameolewa huko Bara, ambao wamewashangaza wengi kwa nidhamu yao ya hali ya juu.
back to top