"WAZIRI WA ELIMU AKAMATWE NA ASHITAKIWE"... MBATIA

Baada ya Serikali kutoa kauli kuhusu mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka jana, Mbunge James Mbatia (NCCR-Mageuzi), ametaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, awajibike na ikiwezekana akamatwe na kushitakiwa. 
Kauli hiyo aliitoa jana kwa waandishi wa habari akisema kuvurugika kwa utaratibu kutokana na kuanzisha utaratibu mpya wa usahihishaji na kutoa alama bila kushirikisha wadau, unamgusa Waziri ambaye ndiye mwenye dhamana. 
Alisema watu wa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA)  hawawezi kufanya uamuzi bila kujulikana na watu wengine wa juu akiwamo Waziri na kusababisha wanafunzi wengi kufeli mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.
Aidha, Mbatia alisema kwa mantiki na falsafa ya utendaji haiwezekani utaratibu huo ukakosa baraka za Waziri wa Elimu.“Si kujiuzulu tu kuna watu wanatakiwa wakamatwe na kushitakiwa kwa kosa hili, kwa kuwa limefanyika kwa makusudi…limetengenezwa, halikutokea kwa bahati mbaya,” alisema.
Mbatia ambaye alifuatana na Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema Dk Kawambwa alitakiwa kwa ripoti ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, asionekane hadharani kwa sababu ni aibu kwake.
Aidha, alisema Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu kuchunguza kufeli kwa wanafunzi hao, imebeba asilimia 75 ya maudhui ya hoja yake aliyoiwasilisha bungeni kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu nchini mwaka jana.

Aidha, alisema ni vema wanasiasa na watu wengine wakakubaliana na ukweli wa kusikiliza hoja na kuacha ushabiki wa kisiasa.

“Hatuwezi kusubiri Rais na Waziri Mkuu kuwa viranja wa kuhakiki mawazo yanayotolewa na wananchi. Mungu anaweza kumtumia mtu yeyote kuleta mabadiliko . La msingi ni taarifa na si mtoa taarifa,” alisema na kuongeza:

 
“Hata mwendawazimu ana haki ya kusikilizwa. Kama hoja yangu ingelipokewa na Bunge, hatua kadhaa nilizopendekeza zingekuwa zimetekelezwa  na Taifa lingejiepusha na aibu hii.”

Aidha, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema ripoti hiyo inaliamsha Bunge kutoka usingizi wa kutumia itikadi za vyama kufanya uamuzi.

Alisema aliyesoma au kusikiliza hoja yake, amethibitishiwa  na ripoti ya Tume ya Waziri Mkuu  kwamba misimamo  ya kiitikadi bungeni ni adui wa maendeleo ya Taifa.
back to top