Tanzania
Dar es Salaam. Mwili wa
mwanafunzi wa Tanzania aliyefia nchini China, Leonard Peter Tambalu
aliyekuwa akisoma Chuo cha Huazhong Agriculture, mjini Wuhan sasa
utawasili leo ukitokea Addis Ababa, Ethiopia.
Awali, habari zilizopatikana juzi zilidai kuwa
mwili huo ungeletwa nchini jana, lakini kutokana na kuunganisha ndege,
ilibidi kulala Addis Ababa.
Tambalu aliyekuwa Ofisa Kilimo Mwandamizi wilayani
Iramba, Mkoa wa Singida, alifikwa na mauti Machi 17 mwaka huu Uwanja wa
Ndege wa Beijing akijiandaa kupanda ndege kuja nchini.
Habari zilizopatikana jana kutoka Beijing, China
zilisema mwili wa Tambalu uliondoka Beijing jana Aprili 9 saa 5:59 usiku
kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kwa ndege namba ET605
iliyotua Addis Ababa saa 2:59 asubuhi. Baadaye ndege itakayochukua mwili
wa Tambalu, itaondoka Addis Ababa leo saa 4:30 asubuhi kwa ndege namba
ET805 inayotarajiwa kufika Dar es Salaam saa 7:25 mchana.
Hivi karibuni, Katibu wa Umoja wa Wanafunzi
wanaosoma vyuo mbalimbali Mji Wuhan (Wtasa), Hamphrey Sikauki alisema
Tambalu alifariki na mwili wake ulikuwa unafanyiwa uchunguzi na maofisa
wa Serikali ya China wakishirikiana.
Wakati huohuo, Jane Tumainieli, aliyekuwa mke wa
Mnadhimu Mkuu Mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
Tumainieli Kihwelu atazikwa leo nyumbani kwake Mbezi Louis.