Akizungumza katika harambee na uzinduzi wa mfuko wa waendesha
pikipiki maarufu mkoani Arusha, Lowassa alisema hiyo ni sera ya CCM
kuwakomboa vijana na kuongeza kuwa kitendo cha wafanyabishara wa Arusha
kujipanga kusaidia bodaboda ni cha mfano kwa wafanyabishara wengine
nchini.
“CCM ni chama kinachotetea wanyonge na nyinyi ni wanyonge
mnaohitaji kunyanyuliwa kimaisha, kitendo hiki cha wafanyabishara wa
Arusha ni kuunga mkono sera ya chama,” alisema.
Lowasaa alirejea tahadhari yake kuwa tatizo la ajira ni bomu linalosubiri kulipuka.
“Tusipowasaidia vijana kuondokana na tatizo hili, amani itatoweka
na ndiyo maana CCM katika Ilani yake ya Uchaguzi imeliweka hilo na pia
kulisisitiza katika vikao vyake vya juu mkutano mkuu pamoja na
halmashauri Kuu,” alisema.
Arusha ni ngome kuu ya Chadema na vijana ndiyo wafuasi wake lakini tukio hilo limeonekana kama kuwateka vijana hao.
Wafanyabiashara maarufu jiji Arusha wakiongozwa na Mjumbe wa
halmashauri Kuu na Diwani wa Mererani, Mathias Manga ndiyo waliyobuni
wazo la kuwaanzishia mfuko vijana wa bodaboda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha waendesha bodaboda mkoani
Arusha, Fabian Shayo, alimpongeza Lowassa kwa kuwa msemaji mkuu wa
tatizo la ajira kwa vijana na kumuomba asikatishwe tamaa na yanayosemwa.
Katika harambee hiyo zaidi ya Sh. milioni 84 zilipatikana, huku
Lowassa pamoja na marafiki zake akichangia Sh. milioni 10 na pikipiki
10.