Wana-CCM 335 Kilwa Masoko watimkia CUF


Prof. Ibrahim
Mwenyekiti wa CUF, Prof.Ibrahim Lipumba
Wanachama 335 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kilwa Kaskazini, wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).

Wanachama hao wamedai kuwa wamelazimika kuchukua hatua kutokana na sera za CCM kutotekelezeka.
Walichukua uamuzi huo wakati wa mikutano mbalimbali ya hadhara iliyofanywa na viongozi wa CUF wilayani humu hivi karibuni.
Mikutano hiyo ya CUF ni utekelezaji wa Operesheni Mchakamchaka hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Kadi za wanachama hao 335, zilikabidhiwa kwa Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba,mwishoni mwa wiki iliyopita alipofanya ziara wilayani humo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzao wakati wa kukabidhi kadi hizo katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mkapa Garden mji mdogo wa Masoko,Yusuf Juma, alisema tangu wawepo ndani ya CCM, hali zao kimaisha bado imezidi kuwa mbaya kunakosababishwa na sera zisizotekelezeka za chama hicho.
Aidha, alisema kitendo cha viongozi wa CCM kutowajali ikiwamo kushindwa kuwatafutia wakulima soko la kuuzia korosho zao, pia kimechangia wao kufikia uamuzi huo.
“Hivi tupozungumza na wewe, korosho zetu tumekopwa na bado hatujalipwa. Hivi umaskini huu na ule usemi wao wa maisha bora kwa kila Mtanzania yapo wapi? Wakati tunatumia nguvu nyingi lakini hakuna kinachopatikana,” alisema.
Kwa upande wake, Mwanahawa Khalifa, alisema elimu waliyoipata kutoka kwa viongozi wa CUF pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kuwatetea wanyonge wakiwamo wakulima, ndicho kilichomfanya aamue kujiunga na chama hicho (CUF).
Akipokea furushi la kadi hizo, Profesa Lipumba aliwapongeza wanachama hao kwa uamuzi waliouchukua wa kujiunga na CUF.
Aidha, Profesa Lipumba aliuagiza uongozi wa Wilaya ya Kilwa kuhakikisha kwamba wanashirikiana nao katika mapambano dhidi ya kuiondoa madarakani CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
back to top