Wachezaji watano wa Yanga walitajwa jana katika orodha ya nyota 22 walioteuliwa na kocha wa Stars, Mdenmark Kim Poulsen na kutolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF); ambao ni Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athuman Idd ‘Chuji’, Frank Domayo na Simon Msuva ambao wote wanaendelea na kambi ya timu yao nchini Uturuki.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, aliiambia NIPASHE jana kuwa hawatawaruhusu wachezaji wao kuondoka Uturuki na kurejea nchini kwa ajili ya Stars huku pia akielezea kushangazwa na na kitendo cha TFF kuwataka wachezaji wao ilhali wakitambua wazi kwamba timu yao (Yanga) iko katika maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi.
Mwalusako alisema kuwa kwa mujibu wa utaratibu, wana haki kugoma kuwaachia wachezaji wao kwani mechi za kirafiki ambazo Stars wanajianda kucheza hazimo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
“TFF wanatambua kwamba tuko katika maandalizi ya Ligi Kuu na tumesafirisha timu yetu kwenda Uturuki kwa ajili ya maandalizi ya ligi hiyo. Timu ya taifa inajiandaa kwa ajili ya mechi ya mwezi Machi (dhidi ya Morocco), kwanini wawahitaji wachezaji wetu kwa muda huu?” Alihoji Mwalusako.
“Sisi (Yanga) tuna mipango yetu, mechi ya Morocco iko mwezi wa tatu… ni mbali mno na tunahofia kuharibu mipango ya benchi la ufundi,” aliongeza Mwalusako.
Taarifa zaidi kutoka Yanga zilidai kuwa ‘Wanajangwani’ wamenogewa na raha wanazopata wachezaji wao katika kambi ya Uturuki na kwamba kama timu hiyo ingekuwa ikiweka kambi maeneo mengine jijini Dar es Salaam, Tanzania, ni wazi kwamba wasingekuwa na jeuri waliyo nayo sasa.
“Klabu imetumia fedha nyingi kwenda kuweka kambi Uturuki… si sawa na kutibua kambi hiyo kwa ajili ya mechi ya Stars ambayo haipo katika kalenda za FIFA na hadi sasa haijulinani ni dhidi ya timu gani,” kilisema chanzo kimoja ndani ya Yanga.
Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura aliliambia gazeti hili jana kuwa wamekuwa na mazungumzo na uongozi wa Yanga kuhusiana na suala hilo.
Alisema kama Yanga watagoma kuwaachia nyota wao kwa ajili ya Stars, shirikisho hilo “litajua cha kufanya.”