BALOZI wa Norway nchini, Ingunn Klepsvik ameonya kuhusu hatari za kugeuza suala la gesi ya Mtwara kuwa mtaji wa kisiasa.
Wakati Norway ikisema hayo, Mkurugenzi wa Uchumi
katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Nyamajeje
Weggoro amesema mgogoro huo utamalizika kwa njia ya mazungumzo na
majadiliano yaliyojaa lugha na kauli laini isiyo na vitisho wala
kuwabeza wananchi.
Katika siku za karibuni, kumekuwa na mijadala,
mizozo na maoni kutoka kwa kada mbalimbali kuhusiana na suala la gesi
hiyo inayopatikana katika eneo la Msimbati, Mtwara.
Akitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Sebastian
Kolowa, Lushoto mkoani Tanga, Balozi Klepsvik alisisitiza kuhusu haja ya
Watanzania kuweka mbele masilahi ya taifa badala ya kuangalia masilahi
ya watu binafsi au taasisi.
“Norway ilipogundua nishati ya petroli
tulikubaliana kitu kimoja kwamba suala hili lisihusishwe na kampeni za
kisiasa. Hii itasaidia kuweka mbali masuala ya rasilimali na siasa,”
alisema.
Balozi huyo alisema gesi ya Mtwara inapaswa
kuwanufaisha wananchi wa Mtwara kwanza kabla ya watu wengine, lakini
masilahi ya taifa lazima yawekwe mbele katika mjadala wa suala hilo.
Klepsvik alisisitiza kuhusu umuhimu wa
kuwashirikisha wananchi katika masuala muhimu ya maendeleo na kueleza
kuwa maendeleo endelevu yanapatikana kwa kuwahusisha watu wa kada zote
hasa wanawake.
Hata hivyo, alisema endapo mambo yatafanyika kwa
utaratibu wake, gesi iliyovumbuliwa inaweza kuwasaidia Watanzania kwa
kiasi kikubwa katika maendeleo yao.
“Tulipogundua gesi na petroli, hatukuwa tunafahamu
lolote, tuliita wageni wakatufanyia kazi ya kuchimba, wakati huo
tulipeleka watu wetu vyuo vya nje kusoma na baada ya miaka 10 sasa
tunashughulika wenyewe na kila kitu kwa manufaa ya taifa zima,” alisema
Klepsvik.
EAC yashauri mazungumzo
Akizungumzia mgogoro huo, Dk Weggoro alisema umetokana na wananchi kutopata elimu ya kutosha kuhusu namna watakavyofaidika na rasilimali hiyo inayopatikana katika eneo lao.
EAC yashauri mazungumzo
Akizungumzia mgogoro huo, Dk Weggoro alisema umetokana na wananchi kutopata elimu ya kutosha kuhusu namna watakavyofaidika na rasilimali hiyo inayopatikana katika eneo lao.
“Mgogoro wa gesi Mtwara utamalizika kwa njia ya
mazungumzo na majadiliano lakini siyo vitisho,” alisema alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya EAC jana.
Alisema haamini kama ni kweli wananchi wa Mtwara
hawataki Watanzania wenzao wafaidike na gesi inayopatikana mkoani humo,
bali wanahofia hatima ya maisha, faida na masilahi yao kutokana na
rasilimali hiyo.
“Viongozi lazima wazungumze, wajadiliane na
kufikia mwafaka na wananchi (wanaMtwara), kuhusu mambo yanayogusa maisha
na masilahi yao. Ni vyema watu ambao maliasili na rasilimali
zinapatikana katika maeneo yao wanufaike kwanza kabla ya wengine.”