Mangula kupokea wanaCCM wapya kutoka vyuo vikuu

Mangula kupokea wanaCCM wapya kutoka vyuo vikuu

Kwa ufupi
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini hapa, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Emanuel Mteming’ombe alisema ziara ya makamu mwenyekiti huyo ni ya siku mbili na imelenga kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa ilani ya CCM mkoani hapa.


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Bara, Philip Mangula leo anatarajia kuwasili mkoani Iringa na kufanya mkutano wa hadhara katika viwanja wa Mwembetogwa mjini hapa huku habari zikieleza kuwa atapokea wanachama wapya kati ya 400 hadi 500.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini hapa, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Emanuel Mteming’ombe alisema ziara ya makamu mwenyekiti huyo ni ya siku mbili na imelenga kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa ilani ya CCM mkoani hapa.
Ziara hii ni ya kwanza kufanyika tangu kuchaguliwa kwake katika uchaguzi wa chama hicho uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana mkoani Dodoma yalipo makao makuu ya CCM Taifa.
“Makamu atawasili kesho (leo) saa sita mchana hapa Iringa na akifika kazi yake ya kwanza itakuwa ni kupokea wanachama wapya wengi wanatoka katika vyuo vikuu vilivyopo hapa mkoani na baada ya hapo atafanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Mwembetogwa na kuzungumza na wananchi,”alisema Mteming’ombe.
Mtemeng’ombe alisema miongoni mwa wanachama wanaotarajia kujiunga na CCM wengi wanatoka katika vyuo vikuu vilivyopo mkoani hapa alivyovitaja kuwa ni Mkwawa ,Tumaini, Ruaha (RUCO) na baadhi yao ni vijana walio katika Manispaa ya Iringa Mjini.
Alisema wanaorudisha kadi kutoka vyama vya upinzani hutumia utaratibu wa kuwapokea lakini hawakurupuki kuwaingiza ndani ya chama hadi wanapofundishwa kanuni za chama,maadili na katiba ya chama na kujiridhisha kuwa wanastahili kuwa wanachama wa CCM.
Alisema sababu za kufanya hivyo ni utaratibu wa chama wenye lengo la kuhakikisha kila mtu anayeingia ndani ya CCM anakuwa amepatiwa mafunzo yanayostahili juu ya namna chama kilivyo na kuahidi kuishi kadri ya kanuni za chama hicho ili wasiwe na utaratibu wa kuhamahama.
Chama cha Mapinduzi mkoani hapa kimetangaza rasmi mikakati yake ya kurejesha jimbo na kutishia kuwatimua katika nafasi za uongozi wenyeviti wa mashina,matawi watakaoshindw a kuonyesha nia ya kurejesha Jimbo la Iringa Mjini ambalo kwa sasa linashikiliwa na Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema.

back to top