MWANAFUNZI aliyejifanya Inspekta Mkuu wa Polisi Jumatatu alizirai mahakamani alipoamriwa alipe dhamana ya Sh500,000.
Mwanafunzi huyo, Jackson Sila Siro, mwenye umri
wa miaka 20, alianguka mahakamani alipoashiriwa na ofisa wa polisi akae
baada ya kuelezwa hayo na hakimu mwandamizi, Lucy Mbugua.
Siro ambaye yuko katika mwaka wa kwanza katika
chuo kimoja cha teknolojia alijikuta taabani baada ya kusimamishwa
kizimbani, kwa kosa la kujifanya ofisa wa polisi anayefahamika kwa jina
la David Mwole Kimaiyo.
“Mshtakiwa anatoka katika familia ambayo haina
mapato makubwa. Naomba korti imwachilie mshtakiwa kwa dhamana anayoweza
kulipa pasipo na matatizo,” alieleza wakili wa mshtakiwa huyo. Alipewa
dhamana ya pesa taslimu Sh500,000. Mshtakiwa aliashiriwa na mmoja wa
maofisa wa polisi wanaomlinda atoke kizimbani.
Baada ya kutoka katika kizimba cha mahakama hiyo,
mshtakiwa alitembea kwa mwendo wa pole pole kutoka kizimbani huku
akitokwa na jasho.
“Mwinue tafadhali mwinue.Mwinue akae. Mtoeni nje
mahala palipo na hewa,” ofisa wa polisi aliamuru baada ya mtuhumiwa huyo
kudondoka na kuzirai.
“Ameanguka tu na kuzirai.Miguu yake haina nguvu,”
ofisa wa polisi alieleza baada ya hakimu kuuliza kuhusu masahibu
yaliyompata mtuhumiwa huyo.
Maofisa wengine wa polisi walijaribu kumwinua
kutoka sakafuni lakini wakashindwa. Walimburuta kumtoa nje. Kwenye
veranda mshtakiwa alitokwa na jasho kisha akaanza kulia.
“Nyamaza, Kimaiyo halii ovyoovyo. Simama si
ulijifanya wewe ni Inspekta Jenerali wa polisi. Wacha kulialia. Kimaiyo
anapambana kama ofisa,” mshtakiwa alifokewa.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya mkasa huo wa
kutaka kujipatia fedha isivyo halali ambapo alieleza kwamba alilazimika
kufanya hivyo kama njia ya kumsaidia ili kupata fedha kw ajili ya
kutatua matatizo yake yaliyokuw ayakimkabili chuoni.