IMEKULA kwake! Wauza nyago kwenye sinema
za Kibongo, Wema Isaac Sepetu na Aunt Ezekiel Grayson wamemuingiza
mkenge staa mwenzao, kaka mkubwa Jacob Steven ‘JB’ baada kukubali
mwaliko kisha kumkatalia dakika za mwisho.
Habari za ndani zilidadavua kwamba JB na
wasanii hao walitakiwa kusafiri kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya
kujifunza utamaduni wa huko ambapo walipelekwa na uongozi wa Ukumbi wa
Princess Cassino uliopo Posta jijini Dar.
Katika hali ya kushangaza, uongozi huo
ukiwa tayari umeshawakatia tiketi za daraja la kwanza (first class)
zinazogharimu kama dola elfu moja (zaidi ya Sh. milioni 1.6) kila mmoja
na baadhi ya wasanii kama Vincent Kigosi ‘Ray The Greatest’ na Amri
Athuman ‘Mzee Majuto’, Wema na Aunt Ezekiel walikataa siku moja kabla ya
safari.
Diza kwenye tasnia ya filamu Bongo, Aunt Ezekiel Grayson.
Chanzo chetu makini kilipenyeza habari
kuwa, Wema na Aunt walichomoa safari hiyo baada ya kuhisi haikuwa na
maslahi kwao na walivyopeleka maombi yao ya kimaslahi kwa JB, aliwaambia
ni safari ya kujifurahisha na hakuna fedha yoyote watakayopata.
Baada ya kuzinyaka habari hizo, Risasi
Jumamosi lilimtafuta Aunt ambaye alikiri kuchomoa safari hiyo baada ya
kushindwana kimaslahi.
“Unajua ile ni kwenda kutangaza biashara
ya mtu kwa hiyo sisi tuliwatajia kiasi cha fedha ambacho tulikitaka
kulipwa lakini tulishindwana ndiyo maana tukakataa kusafiri maana
hatuwezi kufanya kitu ambacho hakina maslahi kwetu na kwenda
kuwafaidisha wengine,” alifunguka Aunt.
Naye Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity,
Steven Mengere ‘Nyerere’ aliilaani safari hiyo na kusema kwamba JB ni
mnafiki kwani aliwachagua wasanii wachache kwa upendeleo ambao baadhi
yao wamemwangusha kwa kutokwenda.
JB.
“Ukweli nimegundua JB ni mbinafsi,
nilikuwa naambiwa lakini nikawa namtetea, sasa nimeamini kwamba hafai
akirudi lazima nitamuita, nitazungumza naye kwa nini aliamua kufanya
hivyo wakati kila kitu kinapotokea iwe safari au vitu vingine huwa sisi
Bongo Movie Unity tunashirikishana lakini kwa hili ameona afanye
mwenyewe,” alisema Steve Nyerere.