Serikali imetakiwa kutoa maelezo
bungeni, kuhusu sababu za kuuawa kwa waasisi sita wa Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar wanaodaiwa kuzikwa katika handaki moja Zanzibar.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano), msemaji wake, Tundu Lissu aliitaka Serikali
kueleza waasisi hao walifanya makosa gani.
Aliwataja waasisi hao kuwa ni Abdallah
Kassim Hanga aliyekuwa Waziri Mkuu, Abdulaziz Twala aliyekuwa Waziri wa
Fedha na Saleh Akida aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na viongozi
waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi, Othman Shariff, Mdungi Ussi na
Jaha Ubwa ambao alisema waliuawa na kuzikwa handaki moja eneo la Kama,
Zanzibar.
Lissu alisema hayo huku akinukuu kitabu
cha ‘Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru’ kilichoandikwa na Harith Ghassany
alichosema kilionyesha jinsi viongozi hao walivyouawa na kuzikwa katika
kaburi moja.
“Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka
kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi
wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja,” alisema Lissu huku
wabunge wakiwa kimya kumsikiliza.
-Mtanzania