MBUNGE AFUTIWA DHAMANA NA MAHAKAMA NA KUAMRIWA KWENDA RUMANDE KWA SIKU 14.....

Picture: Machemli
Salvatory Machemli, Mbunge, Ukerewe
DHAMANA ya  mbunge wa  jimbo la Ukerewe, Salvatory Machemli (CHADEMA) imefutwa na ameamuriwa na mahakama kwenda rumande  siku 14 kwa kuwa wadhamini wake wamekosa sifa baada ya mshitakiwa na wadhamini wake watatu kushindwa kufika mahakamani ili kuwezesha kesi inayomkabili kusikilizwa kama ilivyopangwa.Pia, Mbunge huyo ametakiwa  kuwasilisha  vitambulisho vyake katika kituo cha polisi na amezuiliwa kutoka nje ya wilaya  bila 
kibali cha mahakama.

Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo Faustine Kishenyi ametoa uamuzi huo leo baada ya upande wa mashitaka kuomba mshitakiwa afutiwe dhamana.

Wadhamini ambao ni Shellifu Ngelezya, Max Mhogo na Konsolata Machemli wamepoteza sifa hivyo udhamini wao umefutwa.

Mwendesha mashitaka wa jeshi la  polisi, Inspekta   Samweli Onyango  amesema mshitakiwa kwa makusudi  ameshindwa kufika mahakani  zaidi ya mara tano bila kutoa taarifa wakati  kesi yake  ikitajwa.

Mwishoni mwa mwezi  uliopita, hakimu  huyo aliamuru  mmoja wa wadhamini  wake, Max Mhogo, awekwe rumande siku saba na baada ya kutoka alitakiwa leo (Novemba 6) afike mahakamani hapo na mshitakiwa pamoja na  wadhamini wake.

Katika utetezi wake, Machemli  amesema  ameshindwa kufika  mahakani  kama ilivyopangwa kwa sababu  ya tarehe ya kesi  yake  kuingiliana  na vikao vya Bunge.

Kesi hiyo  imeahirshwa  hadi tarehe  20 mwezi huu .

Mbunge huyo anakabiliwa na kesi ya uchochezi.

Mwendesha mashitaka wa polisi, ASP Denis Rwiza alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa linalomkabili, Oktoba 23, 2011 katika Kijiji cha Nyamanga kisiwani Ukara wakati akiutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CHADEMA.

Alisema mshitakiwa huyo kwa makusudi aliwachochea wananchi kutenda kosa la shambulio kwa kuwaelekeza wachukue uamuzi mgumu wa kuwazuia, hata kushambulia kwa silaha za jadi ikiwemo marungu, mapanga na fimbo afisa yeyote wa polisi atakayekwenda kutafuta watuhumiwa nyakati za usiku kisiwani hapo.

Katika maelezo yake, mwendesha mashitaka huyo wa polisi alisema kipindi hicho ulikuwepo msako wa watuhumiwa wa mauaji ya watu wanne waliouawa na wananchi Desemba 10, 2010 mbele ya maofisa wa polisi kwa tuhuma za ujambazi
back to top