Baadhi ya dawa zilizokamatwa.
CHANZO CHA HABARITimu ya Oparesheni Fichua Maovu (OFM) iling’atwa sikio na chanzo chake chenye maskani jirani na nyumba ya mwanaume huyo.
Chanzo: Haloo naongea na OFM?
OFM: Hapa ndipo penyewe, tukusaidie nini?
Chanzo: Njooni Magomeni-Kimamba kuna jamaa anaitwa Mrema anasambaza dawa za binadamu zilizokwisha muda wake.
OFM: Una uhakika?
Chanzo: Ninyi njooni mfanye kazi yenu na kama mimi ni muongo nifanyeni chochote.
OFM: Oke tuachie kazi.
Askari akikagua dawa zilizokamatwa.
OFM KAZINIIkiwa inarandaranda eneo la tukio, OFM ilitonywa kuwa Mrema na mkewe wamekuwa wakijihusisha na biashara hatari ya kununua dawa za binadamu zilizokwisha muda wake kwa matumizi ya binadamu kisha kuzipaki upya na kuwauzia wenye famasi wanaokula nao dili.
Ilisemekana kuwa dawa hizo ni zile zinazotupwa dampo tayari kwa kuteketezwa, Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar.
Ilidaiwa kuwa wakishakula dili huko dampo na kuzipata, huzipaki upya katika makopo mengine na kuziuza famasi kwa bei ya chini kidogo ukilinganisha na bei halali.
Ilielezwa kuwa jamaa huyo na mkewe kila baada ya wiki moja huwa wanashusha mzigo wa dawa hizo usiku wa manane kisha kupaki na kuziuza bila kujali kuwa ni hatari na wanafanya mauaji kwa raia wasiokuwa na hatia.
Madawa aliyokutwa nayo mtuhumiwa.
POLISIBaada ya kujiridhisha kuwa ni kweli kuna biashara hiyo haramu nyumbani kwa Mrema, OFM iliwataarifu polisi wa doria Magomeni.
Hata hivyo, wakati kikosi kazi ‘kinaliteka’ eneo la tukio, Mrema na mkewe walifanikiwa kutoroka kupitia mlango wa nyuma.
UKAGUZI
Timu hiyo ilimuomba kijana aliyekutwa nyumbani hapo ruhusa ya kuingia ndani ili kukagua kama kuna kitu kama hicho ndipo mambo yakabumburuka kwani mzigo wa dawa mbalimbali ulikutwa ndani.
Walifanikiwa kukuta maboksi mengi ya dawa za binadamu za aina mbalimbali na makopo tupu ambayo hutumika kuwekea dawa hizo.
Mbali na dawa hizo, kulikuwa na lebo nyingi za kutengeneza zilizoonesha muda wa dawa hizo kwisha muda wake kwa kutumia sampo ya zile za halali.
KIJANA AKIRI
Kijana aliyekutwa ambaye alieleza kuwa ni mfanyakazi anayemsaidia Mrema, alikiri mabosi wake hao kufanya biashara hiyo ya dawa ambazo zimepitwa muda wake.
Pia alikiri kuwa kazi ya kupaki dawa hizo hufanyika usiku mnene ili dili lisivuje.
“Mkinikamata mimi mtanionea tu ni baba na mama ndiyo wanafanya kazi hiyo tena huwa wanaifanya usiku wa manane na kuziuza katika maduka ya madawa,” alisema kijana huyo.
PATROO
Hata hivyo, OFM na polisi walizunguka maeneo hayo wakifanya ‘patroo’ kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi 4:30 usiku lakini Mrema na mkewe hawakuonekana.
Baadhi ya dawa zilizokwisha muda wake zilizokutwa nyumbani kwa Mrema ni pamoja na Penizen-V, Artefan 20/120, Amoxicillin, Antibiotics, dawa za sindano na nyingine nyingi.
WAZIRI MWINYI
Juhudi za kumpata Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya kiganjani kutokuwa hewani.
TFDA WANASEMAJE?
Hata hivyo, Ijumaa Wikienda lilizungumza na Msemaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza ambaye alifafanua ni kwa jinsi gani kunakuwa na usimamizi wa hali ya juu katika uteketezaji wa dawa zilizokwisha muda wake.
Alisema kuwa zoezi hilo linapofanyika linahusisha mamlaka zipatazo tano kama polisi, Mamlaka ya Mapato (TRA), manispaa au halmashauri, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na TFDA wenyewe.
Hata hivyo, alishukuru kwa kumjulisha juu ya tukio hilo na kuahidi mamlaka hiyo kulifanyia kazi mara moja.
MASHUHUDA
Wakizungumzia tukio hilo baada ya dawa hizo kukamatwa, mashuhuda walidai kuwa kitendo hicho ni kucheza na maisha ya binadamu.
“Wapo watu wameshakunywa hizi dawa wakijua watapona lakini utakuta wanakufa kwa sababu badala ya kutibu wanaongeza matatizo mengine tena makubwa.
“Hapa kinachotakiwa ili kunusuru watu ni mamlaka husika kuhakikisha zinafanya ukaguzi wa hizi famasi kuondoa tatizo hili kubwa,” alisema Laizer, mkazi wa Magomeni, Dar.
Hadi gazeti hili linakwenda mtamboni wawili hao walikuwa wakisakwa na polisi ili kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
chanzo; GPL.