Hii post ni maalum kwa mashabiki wa mchezaji
Mwinyi Kazimoto wa Simba ambae ndio huyo hapo juu kwenye picha aliyopiga
Qatar akiwa na Raul Gonzalez wa Real Madrid.
Mwandishi wa habari za michezo Shaffih Dauda kupitia shaffihdauda.com ameripoti kwamba wiki
kadhaa baada ya kutoroka nchini na kukimbilia nchini Qatar kwa ajili ya
kwenda kufanya majaribio ya soka la kulipwa, leo hii kiungo wa
kimataifa wa Tanzania na klabu ya Simba Mwinyi Kazimoto amezungumza
rasmi na mtandao huu na kutoa taarifa nzima ya kuhusu sakata lake la
kutoroka.
Akizungumza
kwa njia ya simu kutoka Doha Qatar, Mwinyi Kazimoto kwanza amekiri
kwamba alitoroka kwenda Qatar kwa nia ya kwenda kufanya majaribio,
“Safari yangu ya kuja huku Qatar ilibidi iwe kabla hata sijacheza mechi
ya marudiano na Ivory Coast, lakini kwa sababu nilikuwa na majukumu
nilivumilia nikabaki mpaka nilipocheza mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda,
wakati tukiwa kambini kwa ajili ya mchezo wa pili ikabidi niondoke kwa
sababu siku zilikuwa zinaenda na muda wangu wa kufanya majaribio ukawa
unaisha,”
Alipoulizwa
kama tayari ameshafuzu majaribio aliyoenda kufanya kiungo huyo wa
zamani wa JKT Ruvu alisema “Mwanzoni nilipata vilabu viwili
vinavyoshiriki ligi daraja la kwanza ya huku, lakini nikachelewa
majaribio na hivyo nikakosa nafasi. Baada ya hapo ndipo ikajitokeza timu
ya Al-Markhiya Sports Club – inayoshiriki ligi ya daraja la pili na
ikavutiwa nami na ikafanya mipango ya kunisajili.”
Taarifa
nchini zimeenea kwamba klabu ya Simba imepokea kiasi cha $35,000 kwa
ajili ya kumuuza kiungo huyo, Je Kazimoto anasemaje? “Ni kweli kutokana
na kwamba nilikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Simba ilibidi nitoe
kiasi cha fedha ($40,000 na sio $35,000 kama inavyoripotiwa) kutoka
kwenye ada ya usajili wangu kuununua mkataba wangu uliobakia na Simba.
“Sasa
hivi nimefanikiwa tayari kupata timu hii lakini ndoto yangu ni
kujitahidi na kuweza kucheza ligi ya juu kabisa hapa, vilevile
ningependa kuwaomba radhi watanzania wote na klabu yangu ya Simba kwa
kitendo cha kutoroka, nafasi ya kucheza soka la kulipwa ilikuwa ni
muhimu kwa maisha yangu na sikutaka niipoteze.”