Waziri wa zamani wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mateo Qaresi akitoa maoni
yake juu ya Rasimu ya Katiba Mpya katika kikao cha wajumbe wa Baraza la
Katiba la wilayani Babati, jana.
Babati. Mwanasiasa mkongwe nchini, Mateo Qaresi
ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya
Pili na Tatu, ikiwamo uwaziri na ukuu wa mkoa, amesema Tanzania kama
taifa halina dira wala mwelekeo na matokeo yake mambo yake yamekuwa
yakienda bila utaratibu huku akishauri Katiba Mpya iruhusu Rais
ashtakiwe.
Akitoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya jana,
Qaresi ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Babati amepinga
mapendekezo mengi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akisema ni muhimu Katiba
Mpya itaje dira ya taifa.
Qaresi katika utumishi wake wa umma, amewahi kuwa
Waziri wa Ushirika na Masoko kati ya mwaka 1989 - 1990, Waziri wa
Utumishi, 1996 - 2000 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tangu 2000 hadi Februari
2006.
“Hivi hawa viongozi wanajua tunapoelekea, leo hii ukiulizwa dira yetu ni nini hakuna anayejua, bali tunajiendea tu,” alisema.
Alisema kwa mfano, Wamarekani licha ya kuwa na
vyama viwili vikubwa, lakini dira yao ni ubepari, Wachina au Warusi dira
yao ni ujamaa (ukomunisti) na kwa mataifa yote yanazo dira, lakini
Tanzania dira yake haijulikani.
“Basi, watangaze kama sisi ni mabepari, wajamaa au
waliberali, ili tujue na tufuate misingi hiyo siyo kila kiongozi kuwa
na utaratibu wake, wengine ruksa wengine hivi lazima tubadilike,”
alisema Qaresi.
Rais aondolewe kinga, ashtakiwe
Akizungumzia ibara ya 83 ya Katiba ambayo
inazungumzia kinga za Rais, alisema ni muhimu sasa kuondolewa kwani
marais wamekuwa na viburi , hawashauriki.
Alisema kuna makosa ambayo marais wanayafanya
ambayo yanafaa kushtakiwa, lakini kutokana na kuwa na kinga, imekuwa ni
vigumu kufanya hivyo.
“Katiba ijayo lazima sasa iondoe kinga kwa marais
ili mtu yeyote aweze kumshtaki Rais na hatua za kisheria ziweze
kuchukuliwa,” alisema Qaresi.
Kuhusu hoja za Kundi la G55 ambalo yeye alikuwa
mwasisi na mwanachama la kutaka Serikali ya Tanganyika, alieleza kuwa
Serikali tatu haziwezi kuepukika na kuwataka wanasiasa wakiwamo wa CCM
kuacha ushabiki.
chanzo;mwananchi.
chanzo;mwananchi.