KLABU ya Simba imemzuia kiungo wake mshambuliaji, Mwinyi Kazimoto (pichani juu), kucheza soka la kulipwa nchini Qatar licha ya kuwa amefuzu majaribio.
Kiungo huyo hivi karibuni alitoroka kwenye kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars, iliyokuwa inajiandaa na mechi dhidi ya Uganda na kutimkia nchini huko kwa ajili ya majaribio.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga ameliambia Championi Ijumaa kuwa hivi karibuni walipokea simu kutoka kwa mmoja wa mawakala wa nchini humo ambaye alitangaza ofa.
Kamwaga alisema kuwa uongozi haukuridhishwa na dau hilo na badala yake wamemtaka kiungo huyo kurejea nchini kwa ajili ya kujieleza sababu ya kutoroka kwenye kambi ya Stars na kwenda Qatar bila kupewa ruhusa.
“Kazimoto amefanikiwa kufuzu majaribio Qatar, lakini hatakwenda kucheza soka huko na badala yake atarejea nchini kujieleza sababu ya yeye kutoroka na kwenda huko bila ya ruhusa ya uongozi.
“Kikubwa kilichosababisha ni dau dogo lililotangazwa na mmoja wa mawakala wa nchini humo aliyewapigia simu viongozi,” alisema Kamwaga.