Habari
kamili zilizonaswa na waandishi wetu ni kwamba mwanaume aliyetajwa kwa
jina la Baba Asha alidai kumfumania rafiki yake wa karibu, Baba Tony
akiwa gesti na mkewe (jina linahifadhiwa), tayari kwa kuvunja naye
amri ya sita. Tukio hilo la aibu ya milenia lilijiri katika nyumba
ya kulala wageni ya Pumzika iliyopo maeneo ya Msimbazi Center, jijini
Dar ambapo mara baada ya kumtia mikononi ‘mwizi’ wake ambaye mbali na
urafiki pia ni majirani, ndipo akamchakaza sura vibaya na kumsababishia
kuvuja damu.
Habari za kina zilidai kuwa mke wa Baba Asha alikuwa
bafuni akioga, mara ukaingia ujumbe mfupi ‘sms’ kwenye simu yake ya
kiganjani, ndipo mumewe akachukua kilongalonga hicho na kuufungua ujumbe
huo.
Ilidaiwa kuwa mume alitaharuki kukutana na ujumbe uliokuwa ukimtaka mkewe kwenda Pumzika Guest House kukutana na jamaa huyo.
Iliendelea
kudaiwa kuwa Baba Asha hakuyaamini macho yake, akausoma tena ule ujumbe
na ndipo akagundua sms nyingine nyingi, vocha na fedha za mtandao
alizokuwa akitumiwa mke wake kutoka kwa Baba Tony.
Chanzo
kilidadavua kuwa baada ya kugundua mchezo mzima, Baba Asha akatulia na
kumsubiri mkewe atoke bafuni ili kuliweka sawa suala hilo.
Ilifahamika kuwa mke aliporudi kutoka kuoga, mume
hakuonesha dalili zozote, alichokifanya ni kumwita mkewe na kumwambia
kuwa achague moja, kufungasha kilicho chake, aondoke nyumbani kwake au
amwekee jamaa mtego anaswe ili ajue mke wa mtu ni sumu.
Jibu lilikuwa rahisi kwani alikubali kuweka mtego ili amnase mbaya wake ndipo atamsamehe.
Ilifahamika kuwa ilipita wiki moja kimyakimya
kwani mara ya kwanza Baba Tony alichezwa na machale, alipofika kwenye
gesti hiyo na kumwona mtu anayemfahamu, alimwambia yule mwanamke
waahirishe.
Habari za uhakika ni kwamba wiki iliyopita, Baba Tony
aliingia kwenye kumi nane, akajaa mzimamzima kwenye mtego wa fumanizi
uliowekwa na Baba Asha na mkewe.
Mara
baada ya kuona mwanaume mmoja (Baba Asha) akiwa na askari kwenye gesti
hiyo akihaha, king’ora kililia kwenye akili ya mwandishi wetu ambaye
hakufanya makosa, akamfuata mfumaniaji kwa nyuma hadi aliporuhusiwa
kumfuata mkewe chumbani.
Chumbani mtiti ulikuwa mkubwa ambapo Baba Tony alikutwa kama alivyozaliwa huku mke wa mtu akiwa bado hajavua na ndipo mtiti ukaanza.
Katika purukushani, Baba Asha alimpa kibano ‘mwizi’
wake hadi akamchana usoni na kumng’oa meno ya mbele, jambo
lililosababisha kutokwa na damu nyingi.
Kama hiyo haitoshi, ili
kuthibitisha kuwa mke wa mtu ni sumu, Baba Asha alimchoma jamaa huyo
bisibisi kwenye makalio hadi askari alipoingilia kati na kumchukua
mtuhumiwa kisha akamtoa nje.
Wakiwa nje ya gesti hiyo, Baba Tony
aliomba kujisafisha damu na baada ya hapo alipigwa pingu tayari kwa
kupelekwa Kituo cha Polisi, Pangani, Ilala...
GPL
GPL