Under the Same Sun wataka Katiba iwafanyie haya walemavu wa ngozi

Uongozi wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) wakiwa kwenye picha ya pamoja. Kutoka kulia ni  Makamu Mwenyekiti wa Chavita Wilaya ya Ilala Suleiman Zalala, Gervas Komba (katikati) Katibu, pamoja na Omary Kitingo ambaye ni Mwanachama (Picha na Joseph Zablon)  


MCHAKATO wa kuunda Katiba Mpya bado unaendelea na sasa upo katika hatua ya uundwaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yatakayokuwa na jukumu la kuipitia Rasimu ya Katiba. Kazi hiyo inatarajiwa kuanza Juni mwaka huu.
Pamoja na kuanza kwa mchakato huo wa uundwaji wa mabaraza ya katiba, wananchi wanaendelea kutoa mapendekezo yao yenye lengo la kuboresha mchakato huo wa upatikanaji katiba mpya.
Shirika linalojishughulisha na utetezi wa watu wenye ulemavu la Under The Same Sun ni miongoni mwa wadau wa katiba waliotoa maoni kuhusu mchakato huo ambapo kwa upande wake linasema “lingependa kuona Katiba Mpya inaheshimu, kuzitambua na kulinda haki za Walemavu”.
Meneja Uendeshaji wa Shirika hilo Gamariel Mboya na Mkurugenzi Mtendaji wake Vicky Ntetema wanasema kwa nyakati tofauti kuwa Shirika hilo limejikita katika kutetea watu wenye ulemavu wa ngozi nchini kwa kupitia programu kuu mbili ambazo ni elimu na uhamasishaji.
Kwa kuzingatia majukumu na malengo ya Shirika lao, wanaona vyema Katiba Mpya ikaboresha haki za kibinadamu za watu wenye ulemavu wa ngozi na hali za watu wenye ulemavu mbalimbali nchini.
Usawa na haki za Walemavu
Under The Same Sun inataka Katiba Mpya kutambua na kuweka mkazo juu ya haki na usawa kwa watu wenye ulemavu kwa kutambua mahitaji yao maalumu.
“Watu wenye ulemavu wa ngozi wanahitaji visaidizi katika elimu, visaidizi hivyo ni vikuza maandishi, vitabu vyenye maandishi makubwa (siyo chini ya font 14), nyongeza ya muda katika mitihani iliyochapwa kwa mujibu wa mahitaji yao, kutambuliwa kwa changamoto zao za uoni hafifu pamoja na matatizo ya ngozi,” anafafanua Gamariel Mboya.
Mboya anapendekeza Katiba ijayo ihakikishe kuwa Walemavu wa ngozi wanapatiwa tiba sahihi na huduma ya utambuzi wa viashiria vya saratani ya ngozi na kutibiwa katika hatua za awali.
“Pia ulinzi na usalama kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ni suala linalochafua sura ya taifa kila uchao. Ili kuliondolea taifa sura hii na kuwafanya watu walemavu wa ngozi waishi kwa amani na utulivu, tunapendekeza mfumo wa nyumba kumi uwe wa kiserikali,” anasema na kuendelea;
“Shughuli za upigaji ramli, kuagua, kutambua wachawi, kuroga wengine, kupandisha cheo, kutajirisha watu, mafanikio katika biashara, kushinda uchaguzi, mitihani na kutumia viungo vya binadamu vipigwe marufuku kikatiba,”anasisitiza Mboya.
Wasiyoona na walemavu wa viungo
Watu wenye ulemavu wa kutoona na wale wenye ulemavu wa viungo, wanapaswa kutambuliwa kikatiba kwa kupatiwa mahitaji yao muhimu.
Mahitaji ya wasiyoona yameelezwa kuwa ni urasimishwaji wa maandishi ya nukta nundu (brail) kwenye vitabu, magazeti, mitihani na maeneo mengine ya kitaaluma na masuala ya habari.
back to top