Jinsi gesi ya Mtwara itakavyonufaisha nchi za Afrika Mashariki

  JANUARI 23, mwaka huu, Mkurugenzi wa Uchumi katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Nyamajeje Weggoro alizungumza na waandishi wa habari kuelezea kongamano la kimataifa kuhusu gesi na mafuta linalotarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia leo hadi keshokutwa.

Pamoja na kuzungumzia ko ngamano hilo litakalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Dk Weggoro pia amegusia kwa tahadhari mgogoro wa gesi unaoendelea kati ya Serikali na wakazi wa Mkoa wa Mtwara kuhusu rasilimali hiyo kusafirishwa kutoka mkoani humo kwenda jijini Dar es Salaam.
Anasema kutokana na unyeti wa gesi na mafuta ambayo tayari yamegundulika katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Sekretarieti ya EAC imejipanga kuzingatia uwazi, uadilifu, weledi na elimu ya kutosha kwa wananchi wa nchi wanachama, ili waelewe faida na manufaa watakayopata kupitia rasilimali hizo.
Hata hivyo, Dk Weggoro anasisitiza kuwa faida na manufaa hayo lazima yaanzie na kuo nekana katika maeneo zinakopatikana rasilimali hizo kabla ya kuenea katika ukanda wote wa nchi za EAC.
“Ndani ya EAC tumeweka mipango na mikakati kuhakikisha rasilimali kama gesi na mafuta ambayo tayari yamegundulika ndani ya nchi wanachama yanazinufaisha nchi wanachama. Kwanza kabla ya kufikiria kuisafirisha kwenda nchi zingine, tunakusudia kujenga mabomba ya kusafirisha nishati hiyo kuunganisha nchi zote tano za EAC,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk Weggoro, tayari upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga hadi Mombasa nchini Kenya umekamilika kabla ya kuunganishwa na bomba lingine kutoka Mombasa-Eldoret hadi Kampala, Uganda.
Kutoka Kampala, bomba hilo litajengwa hadi Kigali, Rwanda na baadaye Bunjumbura nchini Burundi. Lengo likiwa ni rasilimali hiyo kunufaisha wananchi wote wa EAC katika uzalishaji wa umeme na bidhaa viwandani.
Fedha kwa ajili ya ujenzi wa bomba kutoka Kigali, Rwanda hadi Bunjumbura, Burundi tayari zimepatikana baada ya Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) kukubali kutoa dola 500,000 za Marekani kugharimia mradi huo huku EAC ikijitahidi kutafuta fedha nyingine za kugharimia ujenzi kutoka Kampala, Uganda hadi Kigali.
“Lengo la EAC ni kuona ujenzi wa bomba kati ya Kampala, Kigali na Bunjumbura unaanza na kukamilika kwa pamoja, ndiyo maana licha ya kupata fedha za kugharimia ujenzi kati ya Kigali-Bunjumbura, hatujaanza utekelezaji hadi tupate za fedha za Kampala hadi Kigali,” anasema Dk Weggoro.

Gesi ya Mtwara
Akizungumzia gesi ya Mtwara na faida yake kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, mtaalamu huyo wa uchumi anasisitiza kuwa gesi hiyo inafaa kutumika kunufaisha Watanzania wote na nchi za EAC kwa jumla, lakini lazima faida hiyo ionekane kwanza kwa wakazi wa Mtwara ambao wana haki ya kujua kila kinachoendelea na namna watakavyonufaika.
“Wanaoishi maeneo yenye rasilimali lazima waone maisha yao na huduma za kijamii kama elimu, afya na miundombinu zinaboreka kutokana na rasilimali zinazopatikana kwao. Siyo dhambi wala ubinafsi wakidai hivyo,” anasema.
Dk Weggoro anasema lazima huduma za kijamii kama shule, hospitali, barabara, nishati ya umeme vipatikane kwa ubora unaolingana na rasilimali zilizoko eneo husika.
Anasema hata huduma na shughuli za kiuchumi kama ujenzi wa viwanda vya bidhaa mbalimbali vijengwe katika maeneo yenye rasilimali na kwamba ni jukumu la viongozi wa Serikali na kijamii kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu fursa zitakazopatikana kutokana na uvunaji wa rasilimali kwenye maeneo yao.
“Elimu hii lazima itolewe kwa wananchi wote kwa kutumia lugha na kauli laini isiyo na vitisho wala mabezo. Elimu hii isitolewe kwa viongozi kama vile wakuu wa mikoa, wilaya, wabunge na madiwani pekee,” anasema Dk Weggoro.
Hata hivyo, anasema haamini kama ni kweli kwamba wananchi mkoani Mtwara hawataki gesi isafirishwe kutoka mkoani humo kwenda Dar es Saalam, hasa kwa sababu pia kuna bomba lingine la gesi linalosafirisha rasilimali hiyo kutoka Songosongo, Lindi kwenda Dar es Salaam.
“Suala siyo gesi kutoka Kusini kwenda Dar es Salaam kwa sababu hata sasa tayari gesi inasafirishwa kutoka huko (mikoa ya Kusini), kwenda Dar es Salaam.Mgogoro wa Mtwara ni matokeo ya viongozi kupuuza ushirikishwaji na elimu kwa umma kupitia lugha na kauli laini zisizo na kebehi wala vitisho kwa wana nchi kuhusu faida watakayopata.”
Anasema hofu hiyo ya wananchi inaweza kumalizwa kwa viongozi kuzungumza, kujadiliana na kufikia mwafaka na wananchi wa Mtwara kwa faida ya pande zote.

Gesi na Katiba
Mgogoro huu gesi Mtwara umetokea wakati Taifa likiwa kwenye mchakato wa kuandika Katiba Mpya ambayo ni sheria mama inayoongoza mambo yote katika jamii yetu. Hivyo ni fursa nzuri kuijadili na kuiwekea utaratibu unaofaa.
Ni fursa nzuri ya kutumia Katiba Mpya kujenga misingi itakayotuongoza katika uvunaji na matumizi ya rasilimali za taifa zilizopo na zitakazogundulika nchini siku zijazo.
Iwekwe misingi imara itakayofuatwa na viongozi wanaposhughulika na rasilimali za taifa. Msingi Mkuu ukiwa ni umma kunufaika kwanza kwa kuanzia na wale wanaoishi maeneo yenye rasilimali.
Kwenye Katiba Mpya, tusikubali watu wanaoishi jirani na rasilimali kama madini, gesi, misitu, hifadhi za taifa na mafuta (utafiti unaendelea), waendelee kutopea kwenye ufukara huku wanaovuna rasilimali hizo (wawekezaji) wakiogelea kwenye utajiri wa kutisha.
Maisha ya wananchi maeneo yenye rasilimali lazima yalandane na thamani ya utajiri unaopatikana maeneo yao na hilo ndilo wanalopigania Mtwara ambayo ni moja ya mikoa maskini nchini.
Baada ya soko la zao la korosho kuporomoka kutokana na sababu mbalimbali, gesi asilia ndiyo ukombozi pekee kwa Mtwara na mikoa ya Kusini. Lazima wajue itakavyowanufaisha na wakidai hivyo hakika siyo ubinafsi wala kuligawa taifa.

Kauli ya Waziri wa Nishati
Nimezungumza kwa nyakati tofauti Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Mhongo na Naibu wake, George Simbachawene. Maelezo yao kuhusu gesi ya Mtwara yanaonyesha faida kadhaa ambayo hakika ikifahamika kwa wana Mtwara, wataruhusu gesi iende Dar es Salaam hata kesho.
Kwa mfano, gesi inayosafirishwa kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ni asilimia 15 pekee ya gesi yote. Asilimia 85 inayosalia itachakatwa na kutumika mkoani Mtwara kwenye viwanda vya mbolea na saruji vitakavyotoa ajira kwa zaidi ya vijana 6,000 wa Mikoa ya Kusini.

Kinachokosekana kwa wana Mtwara ni elimu ya kutosha yenye lugha laini, isiyo na vi tisho wala mabezo.
Viongozi bado wanaishi katika dunia ya kutoa amri na maelekezo ndiyo maana wanadhani kutoa elimu kuhusu gesi kwa wakuu wa mikoa, wilaya, wabunge na madiwani pekee kwa niaba ya wananchi, inatosha.

Tuzingatie ushauri wa Dk Weggoro kuwa, elimu kuhusu mambo yanayowahusu wana nchi itolewe kwa wananchi wenyewe kwenye kata zao, vijiji na vitongoji vyao.
Watawala wajikosoe kwa kurejea kwa wananchi na kuwaelimisha faida itakayotokana na gesi asilia.
Tuzibe ufaa badala ya kusubiri kujenga ukuta. La sivyo, tuta shuhudia ‘Biafra’ kadhaa katika maeneo yenye rasilimali nchini. Mtwara ikionyesha njia.
back to top