Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, Stephen Wassira
Wassira alitua mkoani hapa kusuluhisha mgogoro baina ya Waislamu na Wakristo na kutoa msimamo muda mfupi baada ya kufanya kikao na viongozi wa madhehebu ya dini hizo.
Mbali na kauli hiyo, Wassira aliwataka viongozi wa dini waisaidie serikali katika kuhubiri amani nchini.
Alisema kupitia kikao hicho cha juzi, wajumbe walipendekeza kiundwe chombo maalumu kitakacho kutanisha viongozi wa Kikristo na Waislamu kwa lengo la kuepusha vurugu zinazoweza kusababisha machafuko mkoani hapa.
Alisema chombo hicho siyo lazima kiwe chini ya uongozi wa mkuu wa mkoa na kwamba kitasaidia kufanya mazungumzo kati ya pande hizo kuepuka migogoro.
“Baada ya kukutana na viongozi wa pande zote mbili tumependekeza kwamba suala la uchinjaji kwa ajili ya biashara liendelee kufanywa na Waislamu; na kwamba Mkristo anayechinja kwa ajili ya kitoweo nyumbani kwake asibughudhiwe,” alisema Wassira.
Alisema mbali na hatua hiyo, serikali inaendelea na mazungumzo baina ya viongozi wa pande zote mbili, ili kuepusha machafuko pamoja na uvunjifu wa amani.
Waziri Wassira alisema siyo vyema Taifa likafikia machafuko ama vita kutokana na sababu za imani za dini.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wa kikao kupitia madhehebu ya kikristo walionekana kupokea ushauri huo kwa shingo upande kwa madai kuwa hakuna mwenye uhalali wa kuchinja kuliko mwingine baina ya Waislamu na wakristo.
Mgogoro baina ya waislamu na Wakristo uliibuka mwishoni mwa mwaka jana katika kijiji cha Nyehunge wilayani Sengerema na kusababisha Mkuu wa Mkoa, Ndikilo, kufanya mkutano na wanakijiji hao kwa kuagiza utaratibu wa Waislamu kuchinja kwa ajili ya biashara uendelee.
Kwa upande wao, baadhi ya Wakristo walitaka serikali iruhusu kuwapo kwa maduka ya nyama ambayo imechinjwa na Wakristo.
CHANZO: NIPASHE