TFF kuwasafirisha wachezaji wa Simba kutoka Addis Ababa kwenda Oman.


 Wachezaji sita wa klabu ya simba walioko katika kambi ya timu ya taifa Kili taifa Stars ambayo inajiandaa na mchezo dhidi ya timu ya taifa ya Ethiopia mjini Addis Ababa watasafirishwa na shirikisho la soka nchini TFF kuelekea Oman kuungana na wenzao ambao wanatarajiwa kuanza kambi yao ya wiki mbili nchini humo.
 Akiongea na waandishi wa habari afisa habari wa shirikisho la soka nchini TFF Bonface Wambura amesema shirikisho lake litagharamia usafiri wa wachezaji hao kuelekea Oman mara baada ya mchezo wa Stars dhidi ya Ethiopia na kwamba hayo ni makubaliano baina ya pande mbili hizo.

Wambura amesema kimsingi TFF inatambua safari ya Simba kuelekea nchini Oman kwa ajili ya kuweka kambi ya maandalizi ya timu yao kwa ajili ya mashindano mbalimbali ikiwemo ligi kuu ya soka Tanzania bara pamoja na klabu bingwa Afrika hivyo wamekubaliana kuwasafirisha wachezaji hao kuelekea Oman.

Amesema ingawa kambi ya timu ya taifa itakuwa ikiendelea jijini Dar es Salaam mara baada ya mchezo wa Kili taifa stars na Ethiopia, bado TFF italazimika kuyaheshimu makubaliana hayo.

Amesema kama walivyofanya kwa wachezaji wa Yanga ambao TFF iliwatumia tiketi wachezaji Kelvin Yondan na Frank Domayo, ndivyo watakavyofanya kwa wachezaji wa Simba mara baada ya mchezo huo na kwamba wachezaji hao hawatarejea Dar es Salaam wataelekea moja kwa moja Oman kuungana na kambi ya timu yao ya Simba ambayo inatarajia kuanza hapo kesho.
Baadhi ya wachezaji wa Simba waliko katika kikosi cha Stars kutoka kushoto ni Amir Maftaha, Mwinyi Kazimoto na Amri Kiemba.
 Wachezaji wa Simba walio katika kikosi cha timu ya taifa ni pamoja na nahodha Juma Kaseja, Amri Kiemba, Mrisho Ngasa, Amir Maftaha, Shomari Kapombe na Mwinyi Kazimoto. 
Simba inatarajia kuelekea nchini Oman hii leo kwa maandalizi ya ligi kuu ya soka Tanzania bara pamoja na mchezo wa mzunguko wa kwanza wa michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Recreative de Libobo ya Angola ambao kwa mujibu wa ratiba ya shirikisho la soka barani Afrika mchezo huo utachezwa kati ya Februari 17 na 19.
back to top