Stendi ya Ubungo kuhamia Mbezi Luis kitendawili

 ubungo
Mpango wa Jiji la Dar es Salaam kuhamisha kituo cha mabasi  ya mikoani cha Ubungo (UBT) kwenda  Mbezi Luis, huenda usifanyike kwa wakati  kutokana na maandalizi  kusuasua.
Mbali na maandalizi  ya kukihamisha kuchelewa hali ya upatikanaji wa huduma ndani ya UBT ni duni na wa mashaka  kutokana na halmashauri hiyo kuwaondoa wafanyabiashara.

NIPASHE ilitembelea eneo kitakapojengwa kituo kipya cha Mbezi Luis ambapo hakukuwa na dalili za kuanza ujenzi huo na badala yake eneo hilo limeendelea kuwa na miinuko na vichuguu kuonyesha hakujafanyika maandalizi.
Baadhi ya  majirani wa kituo hicho walidai kuwa kuna wakati waliona tingatinga likisafisha eneo hilo lakini baada ya muda lilisimama na halikuendelea na kazi.
“Mwandishi kama unavyojionea majani yameota ni dalili kuwa shughuli hizo zilisimama muda mrefu,” alisema mkazi  wa Mbezi Mwanaidi Athumani.
Jitihada za kumpata Mkurugenzi wa Jiji, Mussa Zungiza, kutoa ufafanuzi zilishindikana kufuatia maelezo yaliyotolewa na ofisi yake kuwa alikuwa safarini ng’ambo na kuagiza  Ofisa Habari wa Jiji Gaston Makwembe kuelezea ujenzi huo.
Jitihada za kuzungumza na Makwembe hazikufanikiwa kwa vile simu yake haikujibiwa.
Naye Meneja wa Kituo cha UBT Juma Idd, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwani si msemaji.
Mwishoni mwa mwaka jana Mkurugenzi wa  Jiji aliutangazia umma kuwa mchakato wa kuhamisha kituo hicho ungeanza mwaka huu Januari 15 .
Baadhi ya maofisa wa Jiji walielezea hofu yao kuwa   utekelezaji wa tamko hilo hautabiriki.
Kuhusu huduma ndani ya kituo cha UBT, maofisa hao walisema kuwa kinachoendelea kwa sasa ni kusajili wafanyabiashara wapya baada ya kuwaondoa wa mwanzo na kwamba wapya  watafanya biashara zinazohamishika.
Walidai kuwa muda wowote huduma hizo zitarejea hadi  kituo cha Mbezi Lous kitakapokamilika na kwamba kwa sasa wanatafuta mkandarasi atakayekamilisha kazi ifikapo Mei.
Mwishoni mwa mwaka jana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Zungiza, alisema kuwa wanachofanya sasa ni kuwakabidhi viongozi wa mradi wa mabasi yaendayo kasi kubwa  (DART) ili kuendelea na ujenzi wa baadhi ya maeneo ambayo watayateua wao huku kituo kikiendelea na huduma.
Alisema katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa kituo cha Mbezi Luis, utahusu kujenga miundombinu ikiwamo uzio, alama za kuelekeza magari na njia za kuingia na kutoka na kwamba ndani ya miezi mitano kuanzia Desemba mwaka jana, awamu hiyo itakuwa imekamilika.
Mkurugenzi huyo alisema uhamishaji wa kituo  hicho  utategemea kukamilika kituo cha Mbezi Luis.
CHANZO: NIPASHE
back to top