Serikali yasema haina taarifa za upungufu wa madarasa

Mulugo
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo
Wanafunzi 560, 706 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, leo wanaanza masomo yao rasmi leo huku kukiwapo na taarifa kuwa baadhi yao huenda wakachelewa kujiunga na masomo kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa katika baadhi ya mikoa.

Taarifa zinasema kuwa mikoa mingi inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa na kwamba upo uwezekano mkubwa kwa baadhi ya wanafunzi kuchelewa kuanza masomo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,  Philip Mulugo, jana aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu kuwa mpaka sasa hawajapata takwimu za upungufu wa vyumba vya madarasa na kwamba utaratibu wa kupata takwimu hizo utaanza kufanyika wiki hii ili kujua kama kuna upungufu wowote.
“Sisi kama Wizara tunatangaza matokeo, lakini shughuli za kufuatilia taratibu nyingine kama hizo za madarasa na mahitaji mengine zinafanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kwa hiyo kwa kushirikiana nao tutafanya tathmini baada ya shule kuanza wiki hii,” alisema na kuongeza:
“Ni vigumu kubaini kama kuna tatizo, kwa sababu masomo yalikuwa hayajaanza, na ninaamini kwa mwaka huu tatizo halitakuwa kubwa sana kama miaka ya nyuma kwa sababu serikali imekuwa ikijipanga kukabiliana na tatizo hilo.
Mkurugenzi wa Halmashauri Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Fortunatus Fwema, alisema upungufu uliopo katika Halmashauri yake ni ule wa wanafunzin wa awamu ya pili, na kwamba tatizo la vyumba vya madarasa hayo kwa wanafunzi wa awamu ya kwanza halipo.
“Tatizo lililopo ni kwa wanafunzi watakaochaguliwa kwa awamu ya pili ndiyo tunashughulikia na mpaka sasa tunakamilisha vyumba vya madarasa 111,” alisema.
back to top