Mahakama yazuia uongozi wa Jiji Dar usivunje maghorofa

 
Mahakama Kuu. 

Amri hiyo ilitolewa Alhamisi na Jaji, Agathon Nchimbi kufuatia maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa kampuni hiyo, Jerome Msemwa wa Kampuni ya Uwakili ya Msemwa & Company Advocates, chini ya hati ya dharura.


MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara, imeipiga marufuku Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kubomoa wala  kuingilia shughuli za ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa  yanayojengwa na Kampuni ya Silverstone Properties Company Ltd, Oysterbay, Dar es Salaam.
Majengo hayo ambayo yameiingiza matatani halmashauri hiyo, moja linajengwa katika kiwanja namba  321 eneo la  Haile Selassie, lenye urefu wa ghorofa tano na jingine la ghorofa mbili katika kiwanja namba 288, Toure Road Oysterbay, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Amri hiyo ilitolewa Alhamisi na Jaji, Agathon Nchimbi kufuatia maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa kampuni hiyo, Jerome Msemwa wa Kampuni ya Uwakili ya Msemwa & Company Advocates, chini ya hati ya dharura.
Hati hiyo ya dharura inadai suala hilo linahitaji hatua za haraka za mahakama kuingilia kati kwa kuwa mjibu maombi hayo (Jiji) anaelekea kusimamisha shughuli za ujenzi huo kinyume cha sheria wala sababu yoyote inayoeleweka.
Hati hiyo ya dharura pia inadai kuwa kusudio hilo la mjibu maombi ni kinyume cha sheria na masharti ya mkataba uendelezaji na umilikaji wa pamoja wa majengo hayo, baina ya mtoa maombi na mjibu maombi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Kamal Jaffar, katika hati ya kiapo chake iliyoambatanishwa katika maombi hayo namba 4 ya mwaka 2013, kampuni yake iliingia mkataba na jiji,  kujenga na kumiliki kwa ubia majengo hayo. Hata hivyo, anadai kwa sasa halmashauri hiyo inataka kuifukuza kampuni yake katika mradi huo, tena bila taarifa wala sababu za kueleweka, kinyume cha mkataba baina yao.
Katika hoja zake za mdomo mahakamani hapo, Wakili Msemwa alidai kuna tishio kubwa la mjibu maombi (jiji) kutaka kubomoa majengo hayo siku za mwisho wa juma (kati ya Jumamosi na Jumapili), siku ambazo hakuna shughuli za mahakama.
Jaji Nchimbi katika  amri hiyo alisema baada ya kutafakari hiyo za Wakili Msemwa, pamoja na mazingira ya suala hilo, ameridhika kuwa suala hilo linahitaji hatua za haraka za mahakama kuingilia katika kwa madhumuni ya haki.
Hivyo aliamuru pande zote  hali iendelee kuwa kama ilivyo katika majengo hayo kama yalivoainishwa katika hati ya maombi, hadi leo wakati mahakama itakaposikiliza pande zote, huku akiziamuru pande zote kufika mahakamani hapo leo saa 4:30 asubuhi.
back to top