Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa amesema kuwa kuanzia mwaka huu hadi 2015, chama chake kitaipeleka mchakamchaka CCM, kwa kuwa chama chake kimefanikiwa kuwaamsha Watanzania.
Alisema
kwamba Watanzania sasa wameamka na kutambua utajiri wa nchi yao na jinsi rasilimali zinavyotoroshwa nje ya nchi na
kuanza kudai kufaidika nazo kwa nguvu.
Hivyo
Chadema kitaitumia fursa hiyo kuipeleka puta CCM, lengo likiwa kuhakikisha kila
Mtanzania anaishi maisha bora.
Dk Slaa
alisema hayo alipokuwa akizungumza katika kongamano la Umoja wa Wanafunzi wa
Vyuo Vikuu nchini, ambao ni wafuasi wa chama hicho (CHASO), lililofanyika Dar
es Salaam jana.
Alieleza
kuwa kinachotokea mikoa ya Lindi na Mtwara, pamoja na maandamano ya hivi
karibuni ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ni majibu tosha kwa
CCM, kwamba mikutano ya Chadema iliyofanyika mikoa mbalimbali nchini imewaamsha
wananchi.
Wanafunzi
zaidi ya 500 walihudhuria kongamano hilo kutoka
IFM, Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE),
Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu
(DUCE) na Chuo cha Teknolojia Dar es
Salaam (DIT), pamoja na vyuo mbalimbali vilivyopo Dar es Salaam na mikoani.
Desemba 18
mwaka jana Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alisema kuwa mwaka huu
utakuwa ni wa kuunganisha nguvu ya umma kitaifa, baada ya Serikali ya Rais
Jakaya Kikwete kushindwa kuzifanyia kazi hoja mbalimbali zinazotolewa na chama
hicho.
Dk Slaa
ambaye alitumia saa 1:06 kuzungumza na wanafunzi hao, alisema kuwa elimu ya
uraia waliyoitoa kwa wananchi katika mikutano ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C),
pamoja na Operesheni Sangara, wamefanikiwa kwa asilimia 99.
“Tumewapa
elimu ya uraia wananchi katika mikoa yote nchini na sasa wanajua haki zao,’’.Hiyo
ni kazi na mikutano yetu pamoja na maandamano tuliyoyafanya” alisema Dk Slaa na
kuongeza:
“Nawapongeza
wanafunzi wa IFM kwa kuandamana, najua wapo watakaosema nachochea maandamano,
lakini wanatakiwa kujua kwamba wanafunzi hawa walikuwa na haki, haiwezekani
wanabakwa kisha wakae kimya, tena wametoa taarifa polisi na hakuna
kilichofanyika.”
Mbali na
kutaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,
IGP Said Mwema na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
kujiuzulu kwa kitendo cha kuamuru
wanafunzi wa IFM kupigwa wakati walikuwa wakililia usalama wao, alisema
kwamba kuna tofauti kubwa kati ya vurugu na kudai haki za msingi.
“Inakuwaje
polisi wanawapiga mabomu wanafunzi wanaofanya maandamano, lakini wanashindwa
kuzuia Twiga wanaotoroshwa nje ya nchi, tuungane, tushirikiane na tupige
kelele, ili mali zetu zirudi,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Wananchi wa
Mtwara na Lindi sasa wanaandamana kutaka gesi iwanufaishe wao kwanza.
