Baada ya visingizio na ukimya mrefu wa Serikali
kuhusu kurejeshwa nchini kwa mabilioni ya fedha za Serikali zilizofichwa
na baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wa hapa nchini katika benki
za Uswisi, matukio ya hivi karibuni yanaonyesha kwamba sakata hilo sasa
huenda likafikia tamati. Hii ni baada ya Serikali ya Uswisi kutunga
sheria inayowabana walioweka fedha katika benki za nchi hiyo
kuzithibitisha, vinginevyo zitarejeshwa katika nchi husika.
Hizi ni habari njema zinazopaswa kufurahiwa na
raia wote wema siyo tu hapa nchini, bali pia katika Bara la Afrika.
Kihistoria benki za Uswisi zimekuwa zikiendeshwa kwa misingi na sera
zinazoweka kipaumbele katika usiri mkubwa wa akaunti za fedha za wateja
kutoka nchi za kigeni. Bahati mbaya sera hizo zilitumiwa vibaya na
wanasiasa na wafanyabiashara mafisadi na kuziona benki za nchi hiyo
kama vichaka vya kuficha fedha za umma walizopora katika nchi zao.
Katika nchi nyingi barani Afrika, viongozi wa nchi
hizo na washirika wao wamekuwa wakipora fedha za umma na kuzificha
katika benki za nje, hasa za nchini Uswisi. Ipo mifano mingi ya nchi
zenye utajiri mkubwa na rasilimali nyingi kupindukia, lakini wananchi
wake wanaogelea katika lindi la umaskini uliokithiri. Hali hiyo ndiyo
imekuwa moja ya sababu kubwa za machafuko, mapinduzi ya kijeshi na vita
ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi nyingi barani Afrika.
Hapa nchini, suala la ‘mabilioni ya Uswisi”,
ambapo baadhi ya wanasiasa na washirika wao walificha zaidi ya Sh300
bilioni katika benki nchini Uswisi limekuwa kitendawili ambacho
hakijateguliwa. Kama tulivyosema hapo juu, yameanza kupatikana matumaini
ya fedha hizo kurudishwa nchini baada ya Serikali ya nchi hiyo kutunga
sheria ya kuzuia fedha haramu katika benki za nchi hiyo.
Kwa maoni yetu, Serikali yetu ndiyo imekuwa
kikwazo cha kurejeshwa kwa fedha hizo na kutajwa kwa wamiliki wake.
Pamoja na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuwasilisha hoja
binafsi bungeni kuhusu suala hilo na hatimaye Bunge kuielekeza Serikali
kufanya uchunguzi wa kashfa hiyo, bado hatujaona dhamira ya Serikali ya
kuhakikisha fedha hizo zinarudishwa na wahusika wanachukuliwa hatua za
kisheria.
Mbunge huyo sasa yuko Uswisi na ameweza kukutana
na viongozi wa Serikali na kufahamu siyo tu nini kinachoendelea, bali
pia nini kifanyike. Kumbe Serikali ya Tanzania haijaomba taarifa yoyote
kutoka kwa Serikali hiyo kuhusu Watanzania walioficha fedha hizo nchini
humo tangu kuibuka kwa sakata hilo mwaka 2012. Mamlaka za Uswisi pia
zimeweka wazi kwamba Tanzania haijasaini mkataba wa kimataifa wa
kubadilishana taarifa za fedha na kodi. Suala hapa siyo tu kurejeshwa
fedha zilizoporwa na mafisadi, bali pia kuhakikisha fedha safi
zilizowekwa katika benki hizo na Watanzania pia zinatozwa kodi kwa
mujibu wa sheria zetu.
Tunaishauri Serikali isaini mkataba huo haraka
iwezekanavyo. Tayari nchi yetu imepoteza zaidi ya Sh4 trilioni kwa
utoroshaji wa fedha tangu mwaka 2001 na wengi wa watoroshaji hao ni
wanasiasa, vigogo wa jeshi, wakuu wa mashirika ya umma na watendaji
serikalini.
Hapana shaka kikao cha Bunge kijacho kitahakikisha
Serikali inawasilisha ripoti kama ilivyoagizwa na hatimaye litunge
sheria ya kufilisi mali zinazopatikana kwa njia za kifisadi.
CHANZO;mwananchi.
CHANZO;mwananchi.