Wakati mjadala wa usiri wa mishahara ya Rais na
Waziri Mkuu ukiibuka, sasa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anna
Makinda naye ameibuka akidai kuwa mishahara ya wabunge ni midogo kiasi
kwamba wabunge hao huwa na maisha magumu wanapostaafu.
Mjadala wa mishahara ya Rais na Waziri Mkuu
uliibuka baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kuitaja
hadharani alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wilayani Igunga Mkoa
wa Tabora, hivi karibuni.
Zitto alisema Rais analipwa Sh384 milioni kwa
mwaka sawa na wastani wa Sh32 milioni kwa mwezi bila kukatwa kodi, huku
Waziri Mkuu akichukua Sh26 milioni kwa mwezi.
Hatua hiyo imepingwa na baadhi ya wanasiasa,
akiwemo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai akisema
mshahara wa mtu ni siri yake, huku Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya utumishi wa Umma, Celina Kombani akisema ni kinyume cha
sheria.
Nacho Chama cha Watumishi wa Serikali Kuu na Afya
(Tughe), kimekosoa hatua hiyo huku kikitaka Zitto ashitakiwe kwa kutaja
hadharani mishahara hiyo.
Itoshe tu kusema kuwa, bado tuna safari ndefu ya kuikomboa nchi yetu katika lindi la umaskini.
Mishahara ya viongozi wakubwa kama hawa kwa nchi
zilizoendelea iko wazi na wananchi wanaweza kuhoji. Kwetu ni siri kubwa,
siri hii ya nini?
Kwa upande wake Spika Makinda akizungumza na Rais
wa Bunge la Uswisi, Maya Graf aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dar es
Salaam alisema, mishahara ya wabunge ni midogo kiasi kwamba wabunge hao
huishi maisha magumu baada ya kustaafu.
Kutokana na hali hiyo, Makinda alisema wanaandaa mpango wa kuwaokoa wabunge wanapostaafu kwa kuwafundisha ujasiriamali.
Siyo kwamba napinga wabunge kuwa na maisha bora, lakini tulinganishe hiyo inayoitwa mishahara midogo na hali ya maisha yetu.
Hadi mwaka huu, wabunge wetu wanalipwa mshahara wa
Sh11 milioni mbali na posho za Sh330,000 kwa siku ambazo ni sawa na
Sh80,000 ya kujikimu akiwa nje ya jimbo, Sh200,000 ya kuhudhuria kikao
kwa siku na mafuta ya gari ya Sh50,000.
Isitoshe, wabunge hupewa Sh30 milioni ya jimbo kwa
mwaka. Halafu wakimaliza kipindi cha miaka mitano hulipwa kiinua mgongo
cha Sh72 milioni.
chanzo;mwananchi.
chanzo;mwananchi.