
            
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,Jaji Warioba
 
            
Jana tulichapisha habari katika ukurasa wa 
kwanza ikisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeomba kuongezewa muda wa 
mwezi mmoja kutokana na ugumu wa kazi ya uchambuzi wa maoni yaliyotolewa
 na wananchi na asasi mbalimbali. Kama mambo yangekwenda kama 
ilivyotarajiwa hapo awali, Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 1 mwaka jana, 
chini ya Jaji Joseph Warioba ingekamilisha kazi yake Novemba 1, mwaka 
huu.
Kwa mujibu wa Sura ya 83 ya Sheria ya Mabadiliko 
ya Katiba, Tume hiyo ilitakiwa kufanya kazi kwa miezi 18. Hata hivyo, 
Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Augustino Ramadhan alisema juzi 
kwamba wamepeleka serikalini ombi la kuongezewa muda wa kufanya kazi 
kutokana na kukabiliwa na kazi ya ziada ya kuchambua maoni hayo. Pamoja 
na Serikali kukiri kupokea ombi hilo, hadi tunakwenda mitamboni jana 
ilikuwa haijatoa jibu la kulikubali wala kulikataa.
Sisi hatuoni sababu yoyote inayoweza kuisukuma 
Serikali kulikataa ombi hilo, hasa kutokana na kujitokeza kwa mambo 
mengi ambayo hayakutarajiwa kabla na wakati wa mchakato wa Katiba Mpya. 
Mikutano ya Mabaraza ya Katiba iliyofanyika nchi nzima, kwa mfano ilizua
 tafrani kubwa ambapo wajumbe wa mabaraza hayo waligawanyika kwa misingi
 ya kisiasa na kiitikadi. Tume hiyo ililazimika kutumia muda mwingi 
kujielekeza katika kutoa tafsiri na kufafanua vifungu katika Rasimu ya 
Kwanza ya Katiba. Pia Tume ilitumia muda mrefu kuratibu mijadala ya 
Rasimu hiyo, kwani wajumbe wengi wa mabaraza hayo walikuwa wakijadili 
hoja zilizotokana na misimamo ya vyama vyao badala ya kujadili rasimu 
yenyewe.
Hivyo, Serikali haina budi kukubali ombi hilo la 
tume haraka iwezekanavyo, pamoja na ukweli kwamba kuiongezea tume mwezi 
mmoja kuchambua maoni ya wananchi na asasi mbalimbali ni kuongeza 
gharama za mchakato huo. Lakini, wahenga waliposema maji ukiyavulia nguo
 ni sharti uyaoge, walipatia kabisa usemi huo, kwani kama tumeamua kama 
taifa kupata Katiba Mpya itakayotuvusha miaka 50 mingine ijayo lazima 
tubebe gharama hizo za kutuletea demokrasia ya kweli.
Ni vyema tukatambua kwamba hatua ya tume ya kuomba
 kuongezewa mwezi mmoja siyo ya ajabu. Sheria inaipa tume hiyo fursa ya 
kuongezewa miezi miwili nje ya muda uliowekwa. Kinachotakiwa sasa ni 
Serikali kujipanga vizuri na kutekeleza mambo mbalimbali kabla ya 
kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015. Mambo hayo ni pamoja na kuandaa, 
kurekebisha na kupitisha sheria mbalimbali kwa lengo la kuondoa sheria 
kandamizi na kuweka sheria zitakazowezesha kuwapo mazingira linganifu ya
 ushindani wa kisiasa. Kwa mfano, inahitajika sheria mpya ya Tume Huru 
ya Uchaguzi.
Moja ya mambo muhimu ambayo Serikali inapata 
kigugumizi kuyatolea uamuzi ni suala la kufanya uchaguzi wa Serikali za 
Mitaa sambamba na Uchaguzi Mkuu wa 2015. Muda uliobaki kati ya sasa na 
2014 (ambao ulipangwa kufanyika) hautoshi kufanya maandalizi na uchaguzi
 ulio huru na haki. Uchaguzi huo ni vyema usimamiwe na Tume Huru ya 
Taifa ya Uchaguzi. Hivyo, Tamisemi iliyokuwa ikisimamia chaguzi za 
Serikali za Mitaa na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wananchi 
itakuwa imeondolewa mzigo huo mzito. Kufanya uchaguzi huo wakati mmoja 
na Uchaguzi Mkuu kutapunguza gharama kwa kiasi kikubwa kama ilivyo 
katika nchi nyingi barani Afrika na kwingineko.
chanzo;mwananchi.
chanzo;mwananchi.
 
 
