RIPOTI KAMILI: KUMBE DOGO JANJA NA OSTAZ JUMA NAMUSOMA WANATUCHEZEA MCHEZO WA DANGANYA TOTO...

Story ya Dogo Janja kutimuliwa kwenye kampuni ‘inayolegalega’ ya Watanashati Entertainment jana ilivitawala vyombo vingi vya habari nchini. Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Ostaz Juma ambaye hivi karibuni naye alijaribu bahati kwenye muziki kwa kurekodi wimbo uliopotea kwa wiki chache tu, alisikika akihojiwa kwenye vituo vingi vya radio akielezea hatua hiyo.Kuanzia kwenye U Heard ya XXL, Clouds FM, hadi kwenye Showtime ya RFA, Ostaz alisikika akiongea kwa sauti ya msisitizo, kuhusu uamuzi wake wa kumuondoa rapper huyo wa Arusha kundini kwa kile alichodai kuwa amekuwa mtovu wa nidhamu. Wasiwasi wangu juu ya hatua hiyo ilianza mapema tu jana baada ya maelezo ya Ostaz Juma, Dogo Janja na baba yake rapper huyo kukinzana.

Ostaz alisisitiza kuwa amemfukuza msanii huyo kwasababu kadhaa, kubwa likiwa ni suala la nidhamu. Dogo Janja alidai kuwa, hajafukuzwa, bali kajiondoa mwenyewe. Baba yake Dogo Janja alisema hakuwa na taarifa za kufukuzwa kwa mwanae kutoka kwenye kampuni hiyo licha ya Ostaz kuiambia Bongo5 kuwa alishampigia simu kumwelezea uamuzi wake. Baba huyo huyo pia jana aliiambia RFA kuwa waliyaongea jana na wakayamaliza.

Hata kabla ya siku moja haijaisha, leo Ostaz Juma anasema yamekwisha, na amemrejesha kundini.

“Nimeamua kumrudisha, kwa sababu yale mambo yaliyopelekea mpaka mimi kutoa maamuzi yale niliyotoa jana, yaani kawa kama mtu mzima mwenye akili timamu, na mtu yeyote anayelifikiria na akaona kwamba hili ni kosa akasema kwamba ntajirudi, ni kumpa nafasi ya kumsikiliza,” Ostaz ameiambia tovuti ya Times FM.

“Kwa hiyo jana tulikaa kama kikao cha familia nyumbani kwangu, tukazungumza na ni kweli ameona kwamba ni bora aache baadhi ya mambo ambayo hayakuwa mazuri kwenye jamii, na mimi nachokitaka Dogo Janja awe mtu bora, awe mzuri katika jamii. Na yeye ameniahidi kwamba, atawahakikishia watanzania kwamba atakuwa Dogo Janja ambae watanzania wanamtaka wao.”

Naye Dogo Janja ameiambia tovuti hiyo, “Mi niko mtanashati, kwa sababu ni mambo ya kifamilia na tumeshakuwa familia moja, na mimi naona kuhamahama sio swala zuri, na kama nilikuwa na malengo ya kufanya kazi nzuri, ni bora niendelee kupalilia tu hapahapa. Yamekwisha isha kwa ufupi. Kwa namna moja ama nyingine ni ile chuki, marafiki ambao wamenizunguka, ni watu ambao ni soo, sio watu wazuri. Sasa hivi rafiki yangu hela tu.”

Maelezo hayo Ostaz Juma na kauli pamoja na msimamo aliokuwa nao jana na hiki anachokisema Dogo Janja ni ngumu kushawishika kuwa hiki kinachoendelea ni halisi ama ni njia nyingine ya kuendeleza ugonjwa wa kutafuta ‘kiki’ uliopata umaarufu kwenye kiwanda cha muziki cha hapa nyumbani.

Na pengine labda kumshauri tu Ostaz, ni kuwa asipendelee sana kuconclude mambo na kuongea kwa uhakika kwa vyombo vya habari pale ambapo migongano midogo inapotokea ambayo ingeweza kumalizika bila hata nyumba ya jirani kufahamu. Kulikuwa hakuna haja ya jana kutoa kauli ya kumfukuza na tena kwa msisitizo kama huo na kisha leo kuamka na uamuzi mwingine.

Hii inaifanya kampuni ya Mtanashati ionekane ipo kienyeji mno na maamuzi mengine yanafanywa kitoto. Kama ingekuwa ni kampuni iliyodhamiria kufanya kazi kikampuni, basi isingekuwa rahisi kutimua watu kienyeji hivyo na hadi leo kuifanya ibakize wasanii wawili tu, ambao nao hawamake noise yoyote. Pengine ndio maana, Ostaz ameamua kuingia front pia na kufanya muziki. Muziki ambao kwa wengi unaonekana kama utani tu na kejeli kubwa kwa fani hiyo.

Hata hivyo hiyo ni ishara kuwa fungate la Dogo Janja na Mtanashati lina mushkeli mkubwa na nachelea kusema, siku si nyingi watarudi tena hewani wakiongea kile kile kama kilichofanyika jana na kisha baada ya siku chache kurudi tena na kusema wameyamaliza.
back to top