
Wananchi ndiyo wenye kuilea rushwa, ndiyo wenye kuwachagua viongozi
wanaoendekeza vitendo vya ufisadi kila unapofikia wakati wa
uchaguzi.
Baada ya Oktoba 2015, Rais Jakaya Kikwete atakuwa miongoni mwa marais wastaafu wa Tanzania.
Haitakuwa ajabu kumwona akiwa anapunga upepo na
wastaafu wenzake – Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa maeneo ya
Bagamoyo, huku akipokea simu za makada wa CCM watakaokuwa wakiomba
ushauri kwake kuhusu mambo mbalimbali ndani ya chama hicho.
Hatakuwa mwenyekiti tena wa chama hicho na wakati
huo atakuwa akifurahia matunda aliyoyapanda wakati wa utawala wake,
kubwa likiwa ni kuacha Katiba Mpya ambayo upatikanaji wake umetokana na
maoni ya Watanzania.
Rais Kikwete kwa sasa hana cha kupoteza kwa sababu
ndiyo yuko ukingoni kumaliza awamu yake ya pili na ya mwisho ya urais.
Hivi sasa kauli anazozitoa hazina chembechembe za siasa ndani yake,
zinalenga kukikosoa chama chake ili kiweze kuambulia chochote katika
uchaguzi mkuu mwaka 2015, pia zinawalenga Watanzania.
Hivi karibuni, Rais Kikwete wakati akifunga
mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu na wenyeviti wa mikoa na wilaya
wa chama chake alitoa kauli ambayo binafsi nahisi iliwaduwaza vigogo wa
chama hicho.
Alisema kama rushwa haitakomeshwa ndani ya CCM,
katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015, chama hicho kitaanguka
vibaya na iwapo kitanusurika hakitapita kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka
2020.
Kikwete alimpa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philipo Mangula jukumu la kushughulikia viongozi wa CCM wanaokula rushwa.
Rais Kikwete anajua kuwa baadhi ya viongozi wa
chama chake wanakula rushwa, pia anajua kuwa wapo walioshindikana na
ndiyo maana hawajachukuliwa hatua yoyote kwa kuwa wamejenga mtandao
mkubwa kwa kutumia fedha zao.
Hata Mangula naye wamemshinda kwani alipochaguliwa
kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho alikuja na gia mpya katika
uongozi akiahidi ndani ya miezi sita angewang’oa viongozi walioingia kwa
njia za mkato, lakini mpaka leo kimya. Labda hakumaanisha miezi sita
bali miezi sitini.
Nakubaliana na kauli ya Rais Kikwete, lakini kwa
mtazamo wangu nadhani tatizo lipo kwa Watanzania, baadhi yao wakiwa ni
wanaCCM. Leo ukiwauliza watu 10 kwa nini huduma zimekuwa mbaya katika
hospitali zetu, shule, wizarani na kwingineko, watano au zaidi
watakueleza kuwa sababu ni serikali ya CCM kukithiri kwa rushwa.
Wananchi ndiyo wenye kuilea rushwa, ndiyo wenye
kuwachagua viongozi wanaoendekeza vitendo vya ufisadi kila unapofikia
wakati wa uchaguzi.
Nani asiyejua leo hii kuwa mgombea asiyetoa rushwa
kwa wapigakura wake nafasi ya kushinda ni ndogo? Katika mazingira haya
mgombea hawezi kukwepa mtego wa rushwa.
chanzo; mwananchi.
chanzo; mwananchi.