JESHI la Polisi, Kitengo cha Kupambana
na Dawa za Kulevya, linazifanyia uchunguzi wa kina taarifa zinazotolewa
na wadau mbalimbali za baadhi ya watu wakiwemo mawaziri, wabunge na
wafanyabiashara kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.Katika hatua nyingine, jeshi hilo
limesema limechukua hatua mbalimbali katika kudhibiti kushamiri kwa
biashara hiyo nchini, ambapo kiasi cha dawa zilizokamatwa kuanzia
Januari hadi Julai mwaka huu, ni kidogo ikilinganishwa na cha mwaka
jana.
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za
Kulevya cha Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi (ACP), Godfrey Nzowa,
alisema Dar es Salaam jana kwamba jeshi hilo limeongeza mbinu na
mikakati ya kudhibiti biashara ya dawa za kulevya na kuonya kuwa
wahusika wote watakamatwa na kupambana na mkono wa sheria.
“Wapo baadhi ambao tayari tumewahoji na
uchunguzi unaendelea. Ninachokiomba kwa wananchi ni kuwa wasitoe siri
kwa kutumia mitandao ya kijamii, watume siri hizo kwetu moja kwa moja,
maana taarifa zinapotoka kwenye mtandao wahusika wanapoteza ushahidi
haraka,” alisema Nzowa ambaye katika kuthibitisha hilo alisema jeshi
hilo tayari limemhoji Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM) kwa tuhuma za
kujihusisha na biashara hizo.
Kamishna huyo wa Polisi alisema taarifa
za kuwepo kwa wabunge, mawaziri na wafanyabiashara wakubwa
wanaojihusisha na dawa za kulevya, zimekuwa zikifikia jeshi hilo kupitia
vyanzo mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii na kwamba hazipuuzwi bali
zinafanyiwa kazi kwa nguvu kubwa.
Kuhusu Mbunge Azzan ambaye katika siku
za hivi karibuni zimekuwepo taarifa za kudaiwa kujihusisha na biashara
ya dawa hizo, Kamishna Nzowa alisema kwa kifupi; “Idd Azzan tumeshamhoji
na uchunguzi unaendelea.”
Akizungumzia mafanikio ya mwaka huu,
Nzowa alisema kuanzia Januari hadi Julai, Polisi wamekamata kilo 32 za
heroin, kilo 4 za kokeini, kilo 9,999 za bangi, kilo 6,628 za mirungi na
kilo 11 za dawa mpya za kulevya aina ya ephedrine, zilizokuwa
zikisafirishwa kwenda Afrika Kusini.
Alisema katika tukio la heroin
watuhumiwa 44, kokeine watuhumiwa 18, bangi watuhumiwa 1,478, mirungi
watuhumiwa 532 na ephedrine mtuhumiwa mmoja walikamatwa wakiwemo
Wanaigeria watatu na wote wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka.
“Tunawashukuru wananchi wa mikoa
mbalimbali ambao ndio waliotupa ushirikiano uliowezesha kuwakamata
wahusika hawa wa dawa za kulevya ambazo ziliingizwa kupitia katika
viwanja vyetu vya ndege na baharini,” alisema Nzowa.
Alisema vipo viashiria vinavyoonesha
kudhibitiwa kwa biashara hiyo moja ikiwa ni kupungua kwa kiasi
ukilinganisha na takwimu za mwaka jana zilipokamatwa kilo 260 za heroin
na 151 za kokeini, lakini pia kupanda ghafla kwa bei ya dawa hizo
kufikia Sh milioni 50 na milioni 55 kwa kilo moja.
Alisema vita dhidi ya dawa hizo si ya
Tanzania pekee, bali dunia nzima ambapo viongozi wa mataifa mbalimbali
ya ndani na nje ya Afrika wamekuwa wakikutana mara kwa mara kuweka
mikakati ya pamoja ya kukabiliana na biashara hiyo ambayo inawahusisha
watu wenye uwezo mkubwa sana wa kifedha.
“Sasa hivi tupo katika mikakati ya
kuifanya sheria inayohusiana na dawa za kulevya kuwa inayojitegemea
badala ya kuchanganywa na sheria nyingine, lakini pia tunataka kuweka
adhabu kali kwa nchi zote ili mtu anapokamatwa katika nchi yoyote
anakumbana na adhabu kali na si katika nchi nyingine adhabu kuwa ndogo.”
Alisema jeshi hilo limegundua pia kuwepo
mbinu mpya za usafirishaji wa dawa hizo kwa kubadili vifungashio kutoka
katika gundi ya karatasi (selotepu) ya awali na sasa kuwekwa katika
vifungashio vinavyoonesha kuwa ni kahawa halisi, sukari na hata
kuzibadili dawa hizo kutoka katika unga na kuwa vimiminika.