
Kocha Rodgers alikaririwa siku chache
zilizopita akisema kwamba Suarez hatarudi tena katika mazoezi ya kikosi
cha kwanza mpaka atakapoiomba radhi Liverpool pamoja na wachezaji
wenzake kufuatia kauli yake kwamba uongozi wa timu hiyo umemgeuka kwa
kugoma kumuuza kwenda Arsenal.
LIVERPOOL, ENGLAND
NI kifo cha penzi. Uhusiano mzuri na wa kusisimua
baina ya Liverpool na mshambuliaji wake mahiri, Luis Suarez, sasa
unatazamiwa kufa rasmi wiki hii baada ya kubainika kwamba staa huyo wa
Uruguay amegoma kuomba radhi kama kocha Brendan Rodgers anavyotaka.
Watu wa karibu wa Suarez wamesema kwamba kwa sasa
uhusiano wake na Rodgers umekata roho kufuatia mshambuliaji huyo
kutengwa na wenzake katika uwanja wa mazoezi wa Liverpool, Melwood.
Kocha Rodgers alikaririwa siku chache zilizopita
akisema kwamba Suarez hatarudi tena katika mazoezi ya kikosi cha kwanza
mpaka atakapoiomba radhi Liverpool pamoja na wachezaji wenzake kufuatia
kauli yake kwamba uongozi wa timu hiyo umemgeuka kwa kugoma kumuuza
kwenda Arsenal.
Hata hivyo, nyota huyo anashikilia msimamo wake
kwamba mabosi wa wababe hao wa Anfield walimwahidi kumuuza endapo timu
hiyo itashindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Tayari Liverpool imezitolea nje ofa mbili za
Arsenal ambayo ndio timu pekee inayomtaka Suarez huku ofa ya pili ikiwa
imeweka mezani kiasi cha Pauni 40,000,001 ambazo Suarez anaamini
zinatosha kumng’oa Anfield kwa mujibu wa mkataba wake.
Hata hivyo, Rodgers na mabosi wengine wa Liverpool
wamesema hawakuwa na ahadi yoyote ya kumuuza Suarez kwa kiasi hicho cha
pesa na badala yake Rodgers anaamini kuwa nyota huyo ana thamani ya
Pauni 50 milioni na zaidi kama ilivyo kwa mastaa, Edinson Cavani na
Radmel Falcao.
Suarez ameendelea kuwakera mastaa wakongwe
waliowahi kuichezea Liverpool kama John Barnes, Jamie Carragher na
wengineo, huku wengi wakitaka Rodgers amuuze nyota huyo ambaye msimu
uliopita aliifungia timu hiyo mabao 29 katika michuano mbalimbali.
Kitendo chake cha kugoma kuomba msamaha kitaiweka
Liverpool katika wakati mgumu, huku kocha wa Arsenal, Arsene Wenger,
akiendelea kumngoja katika Uwanja wa Emirates.
Nyota huyo anatazamiwa kuitia Arsenal makali ya kutwaa ubingwa kama atafanikisha uhamisho wake.
Sasa huenda uhamisho huo ukaamuliwa katika vyombo
vya sheria vya England endapo Suarez na wakala wake wataamua kuifikisha
Liverpool katika kamati ya Ligi kwa ajili ya kuhitaji msaada zaidi wa
kutia nguvu za kuhakikisha anacheza Arsenal msimu ujao.