
Wanafunzi wa shule ya msingi Hekima waliohudhuria tamasha la kukataa ubakaji lililofanyika hivi karibuni
Ripoti ya hivi karibuni inasema vitendo vya ubakaji
na ulawiti wanavyofanyiwa wanafunzi vimeshika kasi maeneo mbalimbali
nchini, hususan visiwa vya Zanzibar na jiji la Dar es Salaam
Changamoto mbalimbali zinawakabili wanafunzi nchini, hasa wanaosoma katika madaraja ya chini ya elimu.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na
kushamiri kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti, wanavyofanyiwa watoto
chini ya umri wa miaka 18.
Ripoti ya utafiti wa hivi karibuni iliyotolewa na
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), inasema ubakaji umeshika
kasi maeneo mbalimbali nchini, hususan visiwa vya Zanzibar na jiji la
Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliohusu kuangalia
vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, sababu kuu zinazochangia
kuongezeka kwa vitendo hivyo ni umaskini na tamaa iliyopitiliza kwa
baadhi ya wanaume.
Mkurugenzi wa Tamwa Valerie Msoka, anasema ukatili
kupitia ubakaji umekithiri katika maeneo mengi nchini, na vitendo hivyo
hutokea zaidi wanafunzi wanapokwenda shule na hata ndani ya familia.
Wakati ndani ya familia vitendo hivyo vinatajwa
kufanywa na wanandugu, wanafunzi wengi hawana amani hasa wanapokwenda
ama kurudi shuleni kwa kutumia barabara ambazo ni hatarishi. Hawa ni
wale wanafunzi wanaoishi mbali na maeneo ya shule.
“Katika wilaya 10 na vijiji 60 vya Tanzania bara
na Zanzibar vilivyofanyiwa utafiti, inaonyesha kuwa ukatili wa kubakwa
na ulawiti kwa wanafunzi ni mkubwa kiasi cha watoto kukosa fursa yao ya
msingi ya kupata elimu,” anaeleza.
Akirejea baadhi ya tafiti zilizokwishafanywa siku
za nyuma, anasema matukio ya ukatili huo yanasababishwa na mambo kadhaa,
yakiwemo ulevi, imani za kishirikina, umaskini katika familia na tamaa
iliyopitiliza kwa baadhi ya wanaume.
Hata hivyo, anasema juhudi za kupambana na hali
hii zinakosa nguvu, kwani hata matukio yanapotokea na kuripotiwa katika
vyombo vya dola, watuhumiwa hawafikishwi mahakamani.
Aidha, anaeleza kuwa kwa wale wanaofikishwa
mahakamani, huachiwa katika mazingira ya kutatanisha yanayochochewa na
rushwa kwa kisingizio cha kukosekana ushahidi.
“Tatizo lingine ni baadhi ya wananchi kuamua
kusuluhisha tatizo la ubakaji katika ngazi ya familia, kwa madai ya
kuona aibu katika jamii, kutojua haki zao na uelewa mdogo wa sheria
zinazoshughulikia makosa ya ubakaji,” anaongeza kusema.
Ukubwa wa tatizo