
Rais Jakaya Kikwete
VIONGOZI wa nchi mbalimbali za Afrika
wameipongeza Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kupigania utawala
bora Afrika kupitia vita ya ukombozi, kushiriki kutatua migogoro ya nchi
mbalimbali na hata kukubali kupokea wakimbizi.
Pongezi hizo zilitolewa kwa Watanzania kupitia kwa
Rais Jakaya Kikwete mara baada ya kuwa amekamilisha kuwasilisha Ripoti
ya Hali ya Utawala Bora ya Tanzania kwenye mkutano wa Marais wa Umoja wa
Afrika wanaoshiriki katika Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Afrika
(APRM)
Rais Michael Sata wa Zambia ndiye aliyeanza kwa kuishukuru Tanzania wakati akiwasilisha ripoti ya nchi yake katika mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za APRM.
Rais Michael Sata wa Zambia ndiye aliyeanza kwa kuishukuru Tanzania wakati akiwasilisha ripoti ya nchi yake katika mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za APRM.
“Bila mchango wa nchi kama Zambia na Tanzania
katika kupambana na utawala mbovu wa makaburu leo Afrika Kusini
isingekuwa ilipo,” alisema.
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisema wananchi
wa nchi yake hawatausahau mchango wa Tanzania katika kuwakomboa na
kuwafikisha walipo sasa. Tulisaidiwa na nchi nyingi, lakini Tanzania
ilitusaidia kwa namna ya kipekee kabisa.
“Wakati ule wa ukombozi tuliahidi kupitia moja ya
nyimbo za ukombozi kuwa ‘tukiwa huru, hatutakusahau kamwe.’
Nikuhakikishieni kuwa hatutawasahahu,” alisema Rais Zuma akichangia
kuhusu Ripoti ya Tanzania.
Rais Zuma alisema ingawa katika Ripoti ya Tanzania
kuna masuala Serikali inapaswa kuyafanyia kazi kama suala la migogoro
ya ardhi na jinsi ya kuhakikisha kukua kwa uchumi kunawanufaisha
wananchi, Tanzania ina mengi ya kuifunda Afrika na akaeleza utayari wa
nchi yake kuja kujifunza masuala ya udhibiti wa rushwa kwa viongozi na
manunuzi ya umma.
Suala la Muungano lilionekana kumgusa zaidi Waziri
Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegne ambaye alisifu kuwa Muungano
huo unabaki kuwa wa kipekee na unaoikumbusha Afrika juu ya azma yake ya
siku nyingi ya kuunda Umoja wa Nchi za Afrika.
Kwa upande wake Rais wa Senegal Marky Sall alisema
Tanzania ni nchi nzuri na ambayo amepata kuitembelea katika vivutio
vyake vya kitalii kama Ngorongoro na akaenda mbali kwa kuvutiwa namna
Tanzania ilivyorekebisha sheria zake za madini.
Suala la udhibiti wa vurugu za kidini alilokuwa
Rais Kikwete amelizungumzia kwa kina lilimgusa Rais Dk Boni Yayi wa
Benin ambaye alikiri kuwa nchi yake ina tatizo kama hilo na kwamba
angekuwa tayari kujifunza jinsi Tanzania wanavyokabiliana nalo.
Kukamilika kwa uwasilishaji wa Ripoti hiyo sasa
kutaipa nafasi Serikali ya Tanzania kuanza kutekeleza Mpango kazi
unaoainisha jinsi ya kuondoa changamoto za utawala bora zilizobainishwa.