
Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba Jaji warioba
MIKUTANO ya kukusanya maoni kuhusu Katiba Mpya
inayoendelea Visiwani Zanzibar, jana ilifanyika chini ya ulinzi mkali wa
polisi kutokana na vurugu zilizoibuka juzi na kusababisha ivunjike.
Polisi hao, wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliosheheni vifaa vya kijeshi, walionekana wakirandaranda katika mikutano kadhaa, ukiwamo ule uliofanyika katika Shehia ya Matarumbeta, Wilaya ya Mjini Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Baadhi ya askari wa FFU wakiwa na mabomu ya kutoa machozi, bunduki na virungu na wengine waliokuwa wamevalia sare na baadhi ya askari kanzu, walionekana wakirandaranda katika kona za uwanja wa mkutano huo.
Operesheni hiyo ya kutuliza ghasia iliongozwa na Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo, Juma Suleiman na askari hao walikuwa wakimkamata kila mtu aliyeonekana kufanya fujo na katika kamatakamata hiyo, watu kadhaa walipelekwa katika kituo cha polisi cha wilaya hiyo kwa mahojiano.
Kamanda Suleiman alisema jana kwamba watu hao ni miongoni mwa waliokuwa wakishangilia au kuzomea wakati wananchi wakitoa maoni kwa nyakati tofauti.
“Tumewashikilia kwa ajili ya kuimarisha usalama wakati huu wa utoaji wa maoni. Mmoja tumemwachia kwa onyo, lakini mmoja yupo kituoni na huyu pia bado ataendelea kuwa chini ya ulinzi,” alisema Kamanda Suleiman na kuongeza:
“Hata hivyo, baada ya shughuli hii, tutaangalia na kushauriana nini kifanyike kuwafungulia mashtaka au kuwaachia kwa onyo kali.”
Tangu kuanza kwa mikutano ya kutoa maoni ya Katiba Zanzibar, kumekuwa na vurugu zinazohusishwa na mvutano baina ya makundi mawili yenye misimamo tofauti juu ya mfumo wa Muungano.
Makundi hayo ni ya wanaopinga na wanaoukubali. Misimamo hiyo miongoni mwa wananchi imejikita, kulingana na sera za vyama vyao vya kisiasa. Katika misimamo hiyo, CUF kinaamini katika Serikali ya Zanzibar na Tanganyika kila moja ikiwa na mamlaka kamili na muungano wa mkataba, wakati CCM kinasimamia sera ya Serikali mbili; Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, watoa maoni wanaotaka kuwe na serikali tatu; Zanzibar, Tanganyika na Serikali ya Muungano walilalamikia maandalizi ya mikutano hiyo kufanywa na uongozi wa wilaya kupitia viongozi wa Shehia.
Mmoja wa watu hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kasoro iliyopo katika kuandaa mikutano hiyo kupitia shehia ni baadhi ya viongozi wa CCM kuzuia wanaotoa maoni tofauti na msimamo wa chama hicho kutoa maoni. Mikutano ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya Katiba Visiwani Zanzibar, imeingia dosari kutokana na kuvamiwa na makundi ya wanasiasa wanaotaka kupenyeza hoja zao.
Vurugu hizo ambazo chanzo chake ni siasa, zimetokana na wafuasi wa baadhi ya vyama vya siasa, kuvamia mikutano iliyokuwa ikifanyika na kusababisha hofu za kiusalama.
Baadhi ya maeneo ambayo wanasiasa hao walivamia mikutano ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kusababisha ivunjike ni katika Shehia za Magomeni na Mpendae, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika vurugu zilizotokea Mpendae, watu kadhaa walichomana visu baada ya vurugu zilizosababishwa na vijana waliovamia mkutano huo uliokuwa ufanyike jana mchana. Vijana hao walianzisha ghasia hizo kwa kutaka kuvunja utaratibu uliokuwa umewekwa. Walitaka wakae mbele ya wote waliowakuta kwenye mkutano huo. Hatua hiyo ilipingwa na baadhi ya wananchi waliokuwa wamewahi kufika katika mkutano huo na kuzua mzozo uliosababisha watu kadhaa kujeruhiwa kwa visu.