
WANAWAKE wakiwapenda wanaume hubaki na mateso mioyoni mwao.
Hii ni kwa sababu ni vigumu kumtokea mwanaume moja kwa moja kumwaga sera kuwa
unataka ‘akung’oe’.
Ni kweli kwamba, hata kama mwanaume akimkubali mwanamke awe
mpenzi wake baada ya kutokewa, imani yake huwa hafifu kuhusu penzi la kweli la
mwanamke huyo. Anaweza kumtumia kwa siku kadhaa kisha akamwacha. Huo ndiyo
ukweli.
Wanawake waliowahi kuwatokea wanaume wanaweza kuwa na
ushahidi mzuri zaidi juu ya hilo. Pamoja na hayo yote, bado mwanamke anabaki
kuwa binadamu, mwenye hisia za upendo na kutamani baadhi ya vitu.
Anaweza kumpenda mwanaume na ni haki yake ya msingi kabisa.
Kuwa katika uhusiano na mtu unayempenda kwa dhati ni jambo zuri. Moyo huridhia
na kuwa huru katika uhusiano huo.
Hapa katika Let’s Talk About Love tunakupa dondoo
zitakazokusaidia kumsogeza mwanaume ambaye ameuteka moyo wako na hatimaye kuwa
wako moja kwa moja. Katika vipengele vilivyotangulia nilieleza kuwa, kwanza
mwanamke ni vyema ajitunze na aweke mwonekano wake wenye kuvutia muda wote
halafu pia nikaeleza kuhusu kumvutia mwanaume kwa mambo mbalimbali hasa mavazi
na mambo anayopendelea. Sasa tunaweza kuendelea.
ASIWE KWENYE UHUSIANO
Jambo lingine la kuzingatia kwa mwanaume huyo wakati wa
harakati za kumweka mikononi mwako ni kuhakikisha hayupo kwenye uhusiano na mtu
mwingine. Kuna baadhi ya wanawake wapo tayari kuwa na mwanaume hata kama yupo
na mpenzi mwingine; hilo ni kosa na naweza kusema ni umasikini wa kufikiri.
Kama kweli umempenda, itakuwa na maana kama utaweka makazi
ya moyo wako kwake milele na siyo kwa muda mfupi tu.
JISOGEZE ZAIDI
Tayari umeshakuwa na uhakika kuwa hana mtu, sasa unatakiwa
kujisogeza karibu yake. Jizoeshe kumsalimia mara kwa mara na kumsifia kuwa
amependeza.
Kamwe usioneshe dalili kwamba wewe ni ‘maharage ya Mbeya’,
ishia kwenye kujisogeza karibu yake kwa kumsifia na kufanya mambo mengine
yanayofanana na hayo na siyo zaidi ya hapo.
JENGA URAFIKI
Ukaribu wenu sasa unaweza kuwafanya marafiki wa karibu. Kama
uko naye ofisi moja au mnaishi mtaa/nyumba moja ni rahisi zaidi. Kuwa rafiki
yake wa kweli mwenye kujadiliana naye mambo ya msingi.
Katika urafiki wenu, kamwe usiwe mzungumzaji sana (hasa wa
mambo yasiyofaa), aidha usipende kukaa naye katika mazingira yenye vificho
ambayo yataweza kusababisha kuingia kwenye mtego mbaya.
ZUNGUMZIA ZAIDI MAISHA
Kuzungumzia zaidi maisha na kumshauri juu ya mambo muhimu ya
maisha, kutamfanya akuone wewe ni mwanamke makini mwenye malengo mazuri katika
maisha yako. Wanaume wanapenda sana wanawake ambao vichwa vyao vinafanya kazi
sawasawa.
Hii inaweza kuwa sababu itakayomfanya atamani kuwa karibu
yako zaidi, jambo ambalo ndiyo shabaha ya moyo wako.
HAKUNA YEYE BILA WEWE
Kwa sababu tayari ni marafiki na mnashirikiana baadhi ya
mambo, tengeneza mazingira ya kuwa naye karibu zaidi. Mshirikishe kwenye mambo
yako, mfanye ajione si mkamilifu bila kuwa na wewe karibu.
Hili litawezekana kwa kuishika siku yake, kumtakia siku
njema na kumjulia hali yake kazini na maendeleo yake kwa ujumla. Kwa kuwa ni
marafiki, kwa ndani lazima hisia za mapenzi zitaibuka juu yako na utamuweka
kwenye nafasi ya kufikiri kuanzisha uhusiano na wewe.
NI WAKO TU!
Ukipitia hatua zote, bila shaka mwanaume huyo ni wako tu.
Ikiwa pamoja na vyote hivyo bado haonyeshi dalili au hajafunguka kuwa
unamhitaji, basi mwache, siyo riziki yako. Kwa nini ung’ang’anie usipopendwa?