Kwa ufupi
“Serikali lazima ikemee,izuie na ichukizwe na mihadhara ambayo inaleta chokochoko katika taifa letu.”
Dar es Salaam. Mbunge wa
kuteuliwa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ameitaka Serikali kuchukua
uamuzi mgumu wa kuzuia mihadhara ambayo inakashfu dini nyingine na kudai
kuwa ndiyo inayopandikiza chuki miongoni mwa Watanzania.
Akichangia katika makadirio ya bajeti ya Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2013/14, Mbatia alisema Serikali ifike
mahali iseme mihadhara ya kidini sasa basi.
“ Ni lazima tufike mahali tusema mihadhara ya
kidini sasa basi, tuizuie kwa gharama yoyote kama tuna nia njema na nchi
hii,” alisema Mbatia na kuongeza:
Mbatia alisema kuna viongozi ambao hawana nia ya
dhati katika kukomesha tatizo hilo la udini kwani hata katika simu zao
za mikononi zina miito yenye kuonyesha imani zao za dini.
“Kiongozi mzima simu yako ikiita inasikika miito
ya pepo toka pepo toka, ama mingine inasikika miito ya kaswida,
unawaonyesha mfano gani wananchi unaowaongoza,”alisema Mbatia.
Alisema hali hiyo ikiachwa iendelee katika siku
zijazo baadhi ya viongozi watajikuta wakishtakiwa kwenye Mahakama ya The
Hague, Uholanzi kwa kuchochea mauaji.
Alisema amani katika nchi hii ni lazima ilindwe kwa gharama yoyote ile bila kujali wanaofanya hivyo wana imani gani za kidini.
Naye Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alisema ni lazima Serikali
ionyeshe kwamba ipo na inafanya kazi kwa sababu vitendo vya uhalifu
vinazidi kuwatisha Watanzania.
“Hakuna askofu ambaye anaweza kuunda kikundi cha
kihalifu cha kuwadhuru Waislamu, wala hakuna Sheikh ambaye atafanya
hivyo kwa lengo la kuwadhuru Wakristo, wanaofanya uhalifu hawatakiwi
kuvumiliwa,”alisema Selasini.
mwananchi.
mwananchi.